Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Hamdu Shaka, amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si jambo la kisheria pekee bali ni uhalisia wa maisha ya kila siku unaoishi mioyoni mwa Watanzania wote.
Mhe. Shaka alitoa kauli hiyo Aprili 26, 2026 wakati akitoa salamu mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya Chuo cha Ualimu Dawaka, wilayani Kilosa.
Alisema kuwa tarehe 26 Aprili 1964 itabaki kuwa kumbukumbu muhimu katika historia ya taifa, ambapo waasisi Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume walifanya uamuzi wa kihistoria wa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuzaa Taifa la Tanzania.
Alieleza kuwa licha ya kupita kwa miaka 62 tangu kuasisiwa kwa Muungano huo, bado umeendelea kuwa imara, ukiwa umejengwa juu ya misingi ya amani, mshikamano na maendeleo ya pamoja.
“Leo hii Muungano umesimama. Umesimama kwa amani, kwa udugu na kwa maendeleo. Huu si Muungano wa kwenye makaratasi bali ni Muungano wa watu wenyewe,” alisema Mhe. Shaka.
Aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia Muungano huo ni pamoja na kudumishwa kwa amani ya kudumu, kuwa na sauti moja kimataifa pamoja na kuimarika kwa juhudi za maendeleo ya pamoja.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuulinda na kuuenzi Muungano huo kwa vitendo, ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha upendo na kuvumiliana katika jamii.
“Muungano wetu umetupa amani, umetupa utambulisho na umetupa nguvu. Ni wajibu wetu sote kuulinda, kuuenzi na kuuendeleza kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza.
Mhe. Shaka alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kuendelea kushikamana na kudumisha tunu za Muungano ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na mshikamano na ustawi endelevu.





