NA DENIS MLOWE IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevelle, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Kata ya Rungemba ambako amekutana na wananchi wa vijiji vya Kitelewasi na Itimbo kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika ziara hiyo, Lutevelle aliambatana na madiwani, wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji Mafinga pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali za umma.
Kupitia mikutano ya hadhara, alipokea hoja na maswali kutoka kwa wananchi na kuyatolea ufafanuzi huku akibainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kutatua changamoto hizo.
Akihutubia wananchi, mbunge huyo aliwashukuru kwa imani waliyompa na mwonyesha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.
Aliahidi kuendelea kusimamia masuala ya maendeleo, hususan yale yanayohusu kuboresha huduma za jamii katika maeneo yao.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuimarisha miundombinu ya barabara, huduma za maji, upatikanaji wa umeme, pamoja na kuboresha sekta za afya na elimu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Rungemba, Samwel Mwalongo, alimpongeza mbunge kwa hatua ya kutembelea eneo hilo na kusikiliza wananchi moja kwa moja. Alitoa wito kwa wakazi wa Mafinga kuendelea kushirikiana na viongozi wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Ziara ya mbunge huyo inaendelea ambapo leo ataendelea na ziara katika Kata ya Changarawe kwenye vijiji vya Igawa, Block J, Chogo na Lutalawe ambapo atawaeleza wananchi utekelezaji wa miradi mbalimbali na kupokea taarifa za changamoto mpya zinazohitaji ufumbuzi.





