NA FAUZIA MUSSA
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (PSSSF) umesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa majukumu yake pamoja na tofauti iliyopo kati yake na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii, ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza mara kwa mara.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii katika maonesho ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya Mao Zedong mjini Unguja, Meneja wa PSSSF Ofisi ya Zanzibar, Mariam Saleh, alisema maonesho hayo yalitoa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapatia elimu kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo.
Alisema PSSSF ina jukumu la kusimamia malipo ya wafanyakazi pamoja na wastaafu wanaohudumu chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku ikihakikisha taratibu zote za malipo zinafanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazolinda haki za waajiri na waajiriwa.
“Wananchi wengi bado hawajafahamu tofauti ya majukumu kati ya PSSSF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii, hivyo maonesho kama haya yanasaidia kutoa ufafanuzi na kuondoa sintofahamu iliyopo,” alisema Mariam.
Alifafanua kuwa PSSSF ipo chini ya Serikali ya Muungano, wakati Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) unasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), jambo ambalo baadhi ya wananchi hulichanganya.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa PSSSF, Coletha Mnyamani, alisema ushiriki wao katika maonesho hayo ulikuwa na lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kuuliza maswali, kupata elimu ya kina pamoja na kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazohusiana na huduma za mfuko huo.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kutafuta taarifa sahihi kuhusu huduma za hifadhi ya jamii badala ya kusubiri matatizo yatokee, akieleza kuwa elimu ya mapema huwasaidia wafanyakazi kupanga vizuri mustakabali wao wa maisha baada ya kustaafu.
“Tunawaomba wananchi wajenge utamaduni wa kufuatilia haki zao za hifadhi ya jamii mapema, kwani huduma hizi ni msingi muhimu wa ustawi wa maisha ya baadaye,” alisema Coletha.
Maonesho hayo yalizinduliwa rasmi Aprili 23 mwaka huu na Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu historia ya Muungano kuanzia ngazi za awali za elimu.
Alisema hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi chenye uelewa mpana wa misingi ya Muungano, kuongeza uzalendo na kuendeleza maono ya waasisi wa taifa hilo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume.





