NA FAUZIA MUSSA
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk. Riziki Pembe Juma, amewataka wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuulinda, kuuenzi na kuudumisha Muungano wa Tanzania ambao mwaka huu umetimiza miaka 62 tangu kuasisiwa kwake.
Dk. Pembe aliyasema hayo wakati akifunga maonesho ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yaliyofanyika katika viwanja vya Mao Ze Dong, Mjini Unguja, ambapo wananchi, taasisi mbalimbali za umma na binafsi pamoja na viongozi walishiriki kwa pamoja kuadhimisha tukio hilo muhimu la kitaifa.
Alisema kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha Muungano ulioasisiwa na waasisi wa Taifa, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, unaendelea kuwa imara kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alieleza kuwa Muungano uliounganisha Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar umeendelea kudumu kwa miongo mingi kutokana na misingi ya amani, mshikamano na ushirikiano wa wananchi wake, hivyo ni muhimu kuendelea kuulinda dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri umoja wa kitaifa.
Dk. Pembe alisema maonesho hayo yamekuwa ishara ya ushirikiano mkubwa kati ya pande mbili za Muungano, ambapo taasisi mbalimbali zimepata nafasi ya kutoa elimu, huduma na kuonesha mafanikio yao kwa wananchi, jambo ambalo linaimarisha uelewa wa wananchi kuhusu faida za Muungano.
Aliipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha maonesho hayo, akieleza kuwa ushiriki wao umeonesha dhamira ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, aliitaka BOT kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu fursa za kifedha na uwekezaji, ikiwemo ununuzi wa hati fungani za Serikali, ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Pia aliwapongeza washiriki wengine wa maonesho hayo kwa huduma walizotoa kwa wananchi, akisema mchango wao umeacha alama muhimu katika maadhimisho hayo na kuonesha namna taasisi zinavyoweza kushirikiana katika kujenga Taifa lenye mshikamano.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Zanzibar (PSSSF), Mariam Saleh, alisema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo ulikuwa na lengo la kuwahudumia watumishi wa taasisi za Muungano zinazofanya kazi Zanzibar pamoja na kutoa elimu kwa wanachama kutoka pande zote mbili za Muungano.
Alisema maonesho hayo yamewapa nafasi ya kukutana moja kwa moja na wanachama wao, kusikiliza changamoto zao na kuwapatia huduma mbalimbali, huku akibainisha kuwa huduma nyingi sasa zinapatikana Zanzibar pamoja na kupitia mifumo ya kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wake.
Maonesho hayo yaliyoanza Aprili 21 na kuhitimishwa Aprili 26 mwaka huu yakibebwa na kaulimbiu isemayo, “Amani na Umoja ni Msingi wa Maendeleo Endelevu,” kaulimbiu inayosisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa katika kufanikisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.





