Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja,akikabidhi funguo ya pikipiki kwa mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika (Tamcu) Musa Manjaule kwa ajili ya kusaidia utendaji wa kazi mbalimbali za chama hicho
Na Mwandishi maalum,Tunduru
CHAMA kikuu cha ushirika Tunduru(TAMCU) mkoani Ruvuma kwa msimu wa kilimo 2025/2026 kimelipa jumla ya Sh.126,497,586,376.00 kwa wakulima na wadau wengine kwa mazao ya korosho,ufuta na mbaazi.
Hayo yamesemwa jana na meneja wa TAMCU Marcelino Mrope,wakati wa mkutano mkuu wa 23 wa chama hicho mwaka 2026 uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way mjini Tunduru.
Aidha alisema,Tamcu imekusanya na kuuza korosho ghafi jumla ya kilo 41,200,102 zenye thamani ya Sh.102,008,146,090.00 sawa na ongezeko la asilimia 117.7 ya makisio yaliyowekwa ya kilo 35,000,000.00.
Mrope alisema,Tamcu imeendelea kuimarika na kusimamia ubora wa korosho zinazokusanywa ambapo korosho daraja la kwanza zimeuzwa zaidi ya asilimia 98 na daraja la pili zimuzwa chini ya asilimia 1.7na korosho zote zimeuzwa kwenye minada tisa iliyofanyika chini ya usimamizi ya soko la bidhaa Tanzania(TMX).
Kwa mujibu wa Mrope,bei ya juu ya korosho ilikuwa Sh.2,590 ikilinganisha na msimu 2024/2025 ambapo bei ya juu ilikuwa Sh.3,250,bei ya chini 1,266 bei wastani Sh.2,942 wakati msimu 2025/2026 bei ya chini ni Sh.1,610 huku bei wastani Sh.2,475.
Aidha alisema,ili kutekeleza maelekezo ya Serikali,wilaya ya Tunduru iliendelea na mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta na mbaazi ambao umeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima.
“upande wa zao la mbaazi msimu 2025/2026 tulikusanya na kuuza kilo 17,272,495 zenye thamani ya Sh.12,304,389,156 zsawa na ongezeko la asilimia 44.62 ikilinganisha na uliopita ambao uzalishaji ulikuwa kilo 9,565,166”alisema Mrope.
Kwa upande wa zao la ufuta alisema,Chama kikuu kiliendesha jumla ya minada sita ambapo jumla ya kilo 5,042,260 wenye thamani ya Sh.12,185,051,130 na wakulima wamefurahia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa na manufaa makubwa hasa kutokana na bei ya mazao yanayouzwa kwa mfumo huo kuongezeka.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja,ameipongeza Tamcu kwa kutekeleza kwa vitendo dhana halisi ya ushirika kwani kila mwaka chama hicho kimeendelea kufanya vizuri katika kuwahudumia wananchama ambao ni wakulima waliojiunga na ushirika.
Alisema,Serikali ya Mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Tunduru itaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika na wadau wote ili kuhakikisha zao la korosho,ufuta na mbaazi na mazao mengine yanaendelea kuwa chachu ya maendeleo ili kuleta tija kwa wakulima na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika Lima Amcos Rashid Chimata,ameiomba Serikali kuendelea kusimamia bei ya mazao na kutafuta masoko mengi zaidi ili wakulima waweze kupata bei nzuri.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja,akijaribu kuwasha moja ya pikipiki za chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru(TAMCU)zilizotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kusaidia shughuli za chama hicho,kulia Meneja wa CRDB Tawi la Tunduru Emanuel Mwasuka na wa pili kulia meneja masoko wa benki hiyo kanda ya kusini Emanuel Bigamilo.




