Na. John Bukuku- Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akisisitiza kuwa safari iliyoanzishwa si ya mchezo na inalenga mafanikio, hivyo wote ndani ya wizara na wadau wa sekta hiyo wanapaswa kukaa mguu sawa ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Aidha amebainisha kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kutunza vyombo vinavyonunuliwa ikiwemo meli, boti za doria na vifaa vingine vya uvuvi ili viweze kuleta faida kwa taifa.
Ameyasema hayo Aprili 25, 2026 wakati wa uzinduzi wa meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu inayomilikiwa na serikali, hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.
Pia ameongeza kuwa wavuvi wadogowadogo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa mitaji, teknolojia na masoko, ambapo ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na World Bank itaendelea na ujenzi wa masoko pamoja na kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa vijana.
Aidha, Amesema kuwa wizara inapaswa kutoa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha kwa wavuvi ili waweze kunufaika na mapato yao na kuboresha maisha yao.
Aidha amebainisha kuwa ni muhimu kuimarisha mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kufuata sheria na taratibu ili kuhakikisha uwepo wa uvuvi endelevu wenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Pia ameongeza kuwa wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara inapaswa kuendelea kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya uvuvi.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt.Bashiru Ally Kakurwa kuhusu Meli ya Kwanza ya Uvuvi wa Bahari Kuu mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Kigamboni Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2026.





