NIRC Dodoma
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amezindua Baraza la Sita la Wafanyakazi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), huku akitoa wito kwa watumishi wa Tume hiyo kudumisha umoja na kutokubali kukatishwa tamaa na sauti chache za watu wasiothamini kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa baraza hilo, Mhe. Silinde amesisitiza kuwa uongozi ni dhamana ya muda na kila mtumishi ana wajibu wa kutimiza sehemu yake kwa uadilifu kabla ya muda wake kukamilika.
“Kuna watu wachache ambao kila siku wataongea vibaya, lakini msikubali sauti zao ziwafanye mfikiri jamii yote haitaki kazi yenu. Kila mmoja yupo hapa kwa sababu Mungu ana makusudi naye. Sisi sote tunapita tu, hakuna atakayekaa kwenye nafasi yake milele. Muhimu ni kufanya kazi kwa umoja kwa sababu kumkwamisha kiongozi mmoja ni kukwamisha maendeleo ya wananchi,” amesema Mhe. Silinde.
Amesema mafanikio yanayoonekana ndani ya Tume hiyo yanatokana na uongozi imara, uwajibikaji wa watumishi pamoja na ushirikiano wa karibu uliopo kazini, jambo lililoongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake hatua ambayo inaungwa mkono na
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na imai yake ya uwekezaji katika Kilimo cha Umwagiliaji.
“Kilimo ni Umwagiliaji Wizara inabebwa na Umwagiliaji, Rais Dkt. Samia maagizo yake mengi ni kuhusu Umwagiliaji hata hoja Bungeni za Wizara na Waziri Mkuu zinaelekezwa kwa asilimia 80 Umwagiliaji, hii imetokana na taasisi hii kuwa kubwa kwa sasa na kuwa kichochea katika kuongeza uzalishaji na kuwa na Kilimo biashara,”amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, alibainisha kuwa Tume imejipanga vizuri kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kukamilisha, kuendeleza na kusimamia miradi iliyopo huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye uboreshaji wa miradi na ulinzi wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo.
Bw. Mndolwa amesema kumekuwa na changamoto baadhi ya watu wenye fedha kuanza kuwarubuni wananchi na kuwapora maeneo ya ardhi yenye miradi ya Umwagiliaji baada ya kuona Serikali imeweka miundombinu ya kisasa na maeneo hayo yanaenda kuwa na tija.
“Tumeanza kufanya kazi ya kupima maeneo na kuwapa wananchi hati zao ili wasirubuniwe. Ardhi ikipotea leo, haitarudi tena. Tunaiomba Wizara itusaidie kusimamia hili kwa nguvu ili uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais katika Kilimo uwanufaishe walengwa ambao ni wananchi wa kawaida na si matajiri wachache,” amesisitiza Mndolwa.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Saidi Ibrahim, akizungumza katika baraza hilo, amempongeza Mkurugenzi Mkuu na uongozi wake, akimtaja kama mlezi aliyefanikiwa kuimarisha mshikamano kati ya menejimenti na wafanyakazi.
Mhandisi Saidi ameeleza kuwa,Mkurugenzi Mkuu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watumishi wanapata fursa za kujiendeleza kimasomo, kushiriki mikutano na sherehe za kitaifa za wafanyakazi, jambo ambalo awali lilikuwa changamoto.
“Mkurugenzi amekuwa akisimama kama mlezi, akitamani kila mmoja wetu asonge mbele”, alisema Mhandisi Ibrahim.
Aidha, Mhandisi Saidi amewaasa watumishi kutimiza wajibu wao kikamilifu, akisisitiza kuwa “hakuna haki bila wajibu”. Amewasihi watumishi wanaojificha kwenye kichaka cha kutotimiza wajibu huku serikali ikiwa inaendelea na jithiada za kuweka mazingira mazuri ya kazi.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Dkt. Leonia Msafiri, amewahimiza wafanyakazi kujiunga na chama hicho ili kuwa na sauti ya pamoja akisisitiza kuwa mabaraza ya wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kusemea kero na kutafuta suluhu kwa pamoja ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi.
Uzinduzi huo wa Baraza la Sita unatoa mwelekeo mpya wa utendaji kazi ndani ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ikilenga kufikia malengo ya Serikali ya kutoa matokeo chanya katika sekta ya kilimo nchini.





