Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Waziri wa Nchi ofisi ya waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amewataka waajiri na wafanyakazi nchini kuzingatia kwa dhati masuala ya usalama na afya mahala pa kazi ili kulinda nguvu kazi ya taifa na kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesema hayo leo Aprili 23,2026 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 28.
Amesema maadhimisho hayo yanafanyika duniani kote kwa lengo la kuwakumbuka wafanyakazi waliopoteza maisha au kupata ulemavu kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, sambamba na kuhamasisha mbinu za kuzuia ajali hizo.
Ameeleza kuwa siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka 1968 nchini Marekani na baadaye kupanuliwa kimataifa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2001 kwa kuzingatia zaidi kinga na usalama kazini.
Kwa upande wa Tanzania, amesema maadhimisho hayo yalianza rasmi mwaka 2004 na kwa mwaka huu yatafanyika kwa mara ya 23 kitaifa mkoani Njombe, yakiratibiwa na serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kazi.
Amebainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhimiza umuhimu wa mazingira bora ya kazi, hususan afya ya akili, akisisitiza kuwa ustawi wa kisaikolojia wa wafanyakazi ni msingi muhimu wa kuongeza tija na kujenga taasisi imara.
Akitoa takwimu, Waziri huyo amesema zaidi ya wafanyakazi milioni 970 duniani wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili zinazohusiana na kazi, huku ajali na magonjwa ya kazini yakisababisha vifo vya takribani watu milioni tatu kila mwaka.
Amesema hali hiyo inaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa, ambapo dunia hupoteza takribani dola trilioni moja kila mwaka kutokana na kupungua kwa tija na gharama za matibabu.
Aidha, amesema nchini Tanzania
ajali za kazini bado ni changamoto, akitaja kuwa maelfu ya wafanyakazi wamekuwa wakiumia au kupoteza maisha, jambo linalohitaji hatua madhubuti za kuimarisha mifumo ya usalama kazini.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahala pa kazi ili kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa wafanyakazi.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, Waziri amesema kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa wafanyakazi na waajiri, maonesho ya kitaifa, bonanza la michezo, utoaji wa tuzo kwa waajiri bora na huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi.
Ametoa wito kwa wadau wote, wakiwemo waandishi wa habari, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama na afya mahala pa kazi.





