Farida Mangube, Morogoro
RASI wa Ndaki ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Dkt. Nyambilila Amuri amesema chuo hicho kinaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki (Drones) katika kufundishia kilimo cha kisasa.
Anasema matumizi ya drones yanafanyika kwa kushirikiana na kampuni ya Agrimazao, huku akibainisha kuwa teknolojia hiyo imeanza kutumika tangu mwaka jana na inalenga kuongeza uzalishaji, tija pamoja na ufanisi wa matumizi ya pembejeo za kilimo.
Dkt Nyambilila amesema hayo wakati wa mafunzo kivitendo kwa wanachuo wanaosomea shahada za Kilimo katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo,SUA.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Sokoine Profesa Rafael Chibunda anasema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mitaala na kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, huku akieleza kuwa chuo hicho tayari kimenunua ndege nyuki tatu na kinatarajia kuongeza zaidi.
Makamu mkuu huyo wa Chuo kikuu cha Sokoine akasema wameongeza pia Teknolojia ya matrekta chuoni hapo ili kurahisisha kufundishia na wanafunzi kujifunza zaidi Kilimo cha Kisasa na matengenezo ya mitambo ya Kilimo ili kuzalisha wataalamu wengi zaidi.
Wakizungumzia teknolojia hiyo, baadhi ya wanachuo wanasema imewarahisishia ujifunzaji kwa vitendo na kupunguza changamoto za kilimo cha kizamani.
Elizabeth Salim, mwanafunzi wa Shahada ya Uzalishaji wa Mazao na Usimamizi anasema drones zinasaidia kufanya kilimo kuwa rahisi na rafiki kwa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake, Frank Luhanuza anayesomea Uchumi wa Kilimo na Kilimo Biashara anasema matumizi ya teknolojia hiyo yanatoa fursa kwa vijana kujiajiri na kupunguza gharama za uzalishaji, hivyo kufanya kilimo kuwa sekta yenye mvuto zaidi kwa kizazi cha sasa.





