Wizara ya Ujenzi imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji na utoaji wa huduma katika Kitengo cha Mizani nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalaTVma barabarani na kulinda miundombinu dhidi ya uharibifu unaosababishwa na magari yenye uzito kupita kiasi.
Akizungumza baada ya kikao cha mapitio na maboresho ya mifumo ya mizani kilichowakutanisha watumishi wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara (TANROADS), Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde, amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha mizani inafanya kazi kwa ufanisi zaidi kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuimarisha uwazi katika utoaji huduma.
Amefafanua kuwa maboresho hayo yatajumuisha uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu, pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuongeza weledi na uwajibikaji kazini.
Aidha, Dkt. Msonde amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali ili kuhakikisha sheria na kanuni za uzito wa magari zinazingatiwa kikamilifu.
“Lengo letu ni kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara unaotokana na magari yenye uzito kupita kiwango, sambamba na kuboresha huduma kwa wadau wote wa sekta ya usafirishaji,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Mizani Tanzania kutoka TANROADS, Mhandisi Musa George, amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa watafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi, kufanya kazi kwa uadilifu, na kuzingatia sheria na miongozo ili kuboresha utendaji wa mizani nchini.





