Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
Jamii imetakiwa kuendelea kuhamasika kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kufahamu vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha afya zao na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rafael Kwileka wakati wa kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo katika kliniki ya JKCI iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Rafael alisema kupitia kambi hiyo wananchi waliojitokeza wameweza kupata elimu ya mtindo bora wa maisha, kuzingatia lishe bora na namna bora ya kuweza kujikinga na magonjwa ya moyo ili kupunguza gharama zinazotumika kuyatibu magonjwa hayo.
“JKCI sasa tuna kaulimbiu yetu ya jua namba zao za afya ambayo tumeitumia katika kambi hii kuihamasisha jamii kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya shinikizo la damu, sukari kwenye damu, mafuta kwenye damu ambavyo vote hivi vinaweza kusababisha magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Rafael
Dkt. Rafael alisema wamefurahi kuona kupitia kambi hiyo watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea wamejitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa afya kwani watu wenye umri huo ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara.
Aidha Dkt. Rafael alisema kupitia kambi hiyo JKCI kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Damu Salama wameendesha zoezi la uchangiaji wa damu zitakazoenda kutumika kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Venance Mushi aliipongeza JKCI kwa kusogeza huduma karibu kwa wafanyabiasha wa Kariakoo kwani zinawahamasisha kufanya uchunguzi wa afya na hata pale wanapotaka kujisahau kufuatilia afya zao wanakumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko vyote.
“Nawashauri watu wapime afya zao hata mara moja kwa mwaka kwani hakuna kitu kizuri kama kuishi huku unajitambua, tumekuwa bize kuliko afya zetu ndio maana kuna wakati unakuta watu wanaanguka ghafla na wanaowazunguka wanashindwa kujua waanzie wapi”, alisema Mushi
Mushi alisema alitembekea kambi hiyo kwa lengo la kuchangia damu kama ambavyo imekuwa kawaida yake kuchangia damu kila mwaka lakini alivofika katika kambi hiyo akahamasika kufanya uchunguzi wa afya.
“Naipenda sana afya yangu na uwepo wa Taasisi hii katika Soko la Kariakoo imekuwa fursa kwangu kufanya uchunguzi wa afya”, alisema Mushi.
Naye Veronica Innocent mkazi wa Ilala alisema kama kijana amehamasika kufanya uchunguzi wa afya mara baada ya kukutana na kambi hivyo kuwataka vijana wanapokutana na fursa kama hizo wazitumie kuchunguza afya zao.
“Namshukuru Mungu baada ya kufanya uchunguzi wa afya nimekutwa salama na kupewa elimu ya namna naweza kujikinga na magonjwa ya moyo, kuanzia leo nitaishi kwa kufuata elimu niliyoipata hapa”, alisema Veronica




