Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuhakikisha kuwa watanzania wote wanaendelea kuishi katika mazingira bora na salama.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yussuf Masauni wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni jijini Dodoma.
Alisema Ofisi imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191, kutoa elimu kwa umma kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira, kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyenzo mojawapo ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhamasisha upandaji miti, na uwekezaji katika biashara ya Kaboni.
Mhe. Masauni aliongeza kuwa katika kutekeleza Mpango Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Ofisi imeendelea kuratibu upatikanaji wa fedha kupitia mifuko ya kimataifa ya Mazingira ya kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi ili kutekeleza miradi mbalimbali.
Kwa upande wa Muungano, alisema Ofisi imeendelea kuratibu masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika mambo yasiyo ya Muungano.
Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kufanya mapitio na kuchapisha Mwongozo mpya wa Vikao vya Kamati ya Pamoja kati ya SJMT na SMZ, Toleo la 2025. Mwongozo huo pamoja na mambo mengine umeainisha jukumu la kujadili masuala mengine yenye maslahi mapana ya pande mbili ikiwemo fursa zilizopo pande mbili za Muungano na si kujadili hoja za Muungano pekee.
Aidha, alisema katika kuhakikisha kwamba Muungano unaimarishwa kupitia michezo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar na Wizara zenye dhamana ya michezo kutoka pande zote mbili za Muungano pamoja na Mashirikisho ya Vyama vya Michezo Tanzania (TFF na ZFF) tumefanikiwa kurejesha mashindano ya Muungano kwa Mpira wa Miguu yaliyokuwa yamesimama kwa miaka 20.
Kwa mwaka huu mashindano haya yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 21 hadi 29 Aprili, 2026 na yatahusisha timu nane za Simba, Yanga, Azam, Singida Black Stars, Mlandege FC, Mwembe Makumbi City, Mafunzo SC na KVZ FC).




