Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya LIAONING FANGDA kutoka China inayotaka kuwekeza nchini

Mhe. Maghembe alikutana na ujumbe jijini Dodoma Machi 31, 2026.

Ujumbe huo upo nchini tangu Machi 25, 2026 na umetembelea Zanzibar, Dodoma na Dar es Salaam kufanya mazungumzo na viongozi na watalaam mbalimbali ili kujionea fursa za uwekezaji katika sekta ya Afya, Usafirishaji wa Anga, na Madini. 

Ujumbe wa Kampuni hiyo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Ao Xinhua. 

Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Maghembe aliwashukuru kwa kukubali mwaliko wa Serikali kuja nchini kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na kuahidi kuwa Serikali itashirikiana nao bega kwa bega ili kufanikisha azma hiyo.

 Ujumbe huo umeishukuru Serikali kwa ushirikiano waliopata na kuahidi kuwa watarudi Tanzania kuja kuwekeza.

Ujio wa ujumbe huo nchini ni mafanikio chanya ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (MB.), aliyoifanya nchini China mwezi Juni 2025 na kukutana na viongozi wa Kampuni hiyo.