Bw. Rahim Bhanj, Mkurugenzi wa Bhanj Transport Ltd na Mlezi pamoja na Mshauri wa Chama cha Wauzaji na Wasafirishaji wa Makaa ya Mawe nchini, akiwasilisha maoni ya wachimbaji na wasafirishaji uliofanyika jijini Dodoma
Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Akiwasilisha maoni ya wachimbaji na wasafirishaji, Mlezi na Mshauri wa Chama cha Wauzaji na Wasafirishaji wa Makaa ya Mawe nchini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bhanj Transport Ltd, Bw. Rahim Bhanj amesema kuwa kuna umuhimu wa kufanyika marekebisho ya mfumo wa tozo ili zipunguzwe na kuishia mipakani, hatua itakayopunguza gharama katika mnyororo mzima wa biashara.
Aidha, ameishauri Serikali iangalie mfumo tofauti na uliopo sasa, akieleza kuwa kwa wazo lake tozo hizo zingefikia mwisho katika maeneo ya mipakani kama wanavyofanya Australia na South Africa.
Ameyabainisha hayo machi 30,2026, Jijini Dodoma,katika kikao Cha waziri wa madini na wadau wa makaa ya mawe.
Amesema kuwa soko la Uganda ni kubwa na linaweza kuongezeka maradufu, akibainisha kuwa Tanzania inaweza kubaki kuwa msambazaji mkuu wa makaa ya mawe katika soko hilo.
Aidha, amebainisha kuwa viwanda vingi nchini vinatumia makaa ya mawe ya Tanzania huku akieleza kuwa hata wazalishaji wa Kenya wanatumia makaa hayo, na kwamba alipokutana na wadau wa Uganda alibaini wanatumia kuni katika viwanda, jambo lililomfanya kuwashawishi kutumia makaa ya mawe badala yake na wakakubali.
Aidha, ameishauri Serikali kuangalia namna ya kuweka mfumo wa Royalty assessment ili kusaidia kuboresha sekta hiyo.
Mlezi na mshauri wa chama cha wauzaji na wasafirishaji wa makaa ya mawe nchini, Bw. Rahim Bhanj ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bhanj Transport Ltd katikati pichani akizungumza na Waziri wa madini Mhe.Antony Mavunde wapili kutoka kulia katika mkutano wa kwanza wa wauzaji na wasafirishaji wa makaa ya mawe uliofanyika jijini Dodoma.
