NA DENIS MLOWE, IRINGA
MAMIA ya wananchi, viongozi wa dini, siasa, biashara na sanaa wamejitokeza kumuenzi maisha na mchango wa aliyekuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu William Lukuvi ambaye amefariki dunia na kuacha simanzi kubwa katika Taifa.
Katika hotuba zao, viongozi mbalimbali wamezungumza kwa hisia, wakitathmini maisha, utumishi, uzalendo na urithi wa kazi kubwa alizofanya kwa taifa na kwa mkoa wa Iringa.
Peter Msigwa: “Tumepoteza kiongozi wa kipekee, mzalendo wa kweli”
Mchungaji Peter Msigwa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini, amesema taifa limepoteza mtu muhimu ambaye alisimamia majukumu yake kwa uzalendo na weledi wa hali ya juu.
Amesema wizara ya ardhi miaka mingi ilikumbwa na migogoro isiyomalizika, lakini chini ya uongozi wa Lukuvi, kulikuwepo mageuzi makubwa yaliyopunguza kero kwa wananchi.
 “Decentralization ya hati ni moja ya kazi kubwa aliyofanya. Zamani hati zilikuwa zinapatikana Dar es Salaam pekee, baadaye kanda, lakini yeye aliweka mfumo wa kila mkoa kutoa hati. Hili halipaswi kusahaulika.”
Amesisitiza kuwa Lukuvi alikuwa akiamini katika upangaji bora wa miji, akitoa mfano wa Iringa Mjini kuwa moja ya maeneo ya kwanza nchini kuanzishiwa master plan chini ya uongozi wake.l
MFANYABIASHARA Fred Ngajilo maaruufu kama Fred Vunja bei amesema “Tumepoteza mwalimu, mshauri na mwanafalsafa”
Mfanyabiashara maarufu Fred Ngajilo ameuelezea msiba huu kama pigo kwa watu wote waliowahi kufaidika na busara, unyenyekevu na uadilifu wa Lukuvi.
 “Huyu hakuwa mti wa kawaida kuanguka; alikuwa mbuyu. Alikuwa mwalimu, mshauri, na mtu wa falsafa. Wengi tumepitia mikononi mwake, ametuongoza, ametushauri na kutupa mwelekeo.”
Amesema marehemu alikuwa mpenda maendeleo, aliyekuwa akisisitiza elimu, michezo, miundombinu na ustawi wa jamii, akisisitiza kuwa kazi na alama zake haziwezi kufutika
MSANII Steve Nyelele (Steve Mengele): “Tumeondokewa na mlezi wa taifa, sio wa sekta moja”
Kwa niaba ya wasanii wote nchini, Steve Nyelele amesema marehemu Lukuvi alikuwa mlezi wa sekta nyingi na mtu aliyekuwa rahisi kufikika tofauti na viongozi wengine.
“Huyu alikuwa kiongozi wa hadhi ya juu, mtu wa watu, aliyekuwa akisikiliza kila kada. Amewahi kutuita wasanii Dodoma ili kusikiliza changamoto zetu. Tumepoteza mlezi, tumepoteza baba.”
Ameongeza kuwa Iringa imepoteza “kitambulisho chake,” kwani jina la Lukuvi lilikuwa hutajwa sambamba na mkoa hu
NayevMjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa , Arif Abri: anasema “Isimani imepoteza mzazi na nguzo ya maendeleo”v
Arif Abri, amesema jimbo lake na Taifa kwa ujumla limepoteza mtu aliyekuwa msingi wa siasa, maendeleo na ustawi wa jamii.
Amesema miradi mikubwa kama barabara za mkoa, sekta ya maji (mradi wa Pawaga), miundombinu ya VETA, hospitali ya wilaya, na ongezeko la shule za sekondari ni miongoni mwa kazi zilizofanywa chini ya usimamizi wa marehemu.
 “Kutoka shule moja hadi zaidi ya 16, kutoka zahanati hadi vituo vya afya, kutoka changamoto za maji hadi mradi wa bilioni 58 haya yote yanaonyesha alama ya Lukuvi.”
JIMSON KISIGO – MFANYABIASHARA
Amesema “Mtu wa unyenyekevu, msikivu na mwenye busara”
Mfanyabiashara Jimson Kisigo amesema Lukuvi amekuwa nguzo ya vijana katika biashara, akiwafungulia milango na kutoa ushauri katika nyakati muhimu.
 “Nilipokwama kwenye mradi wangu, alinielekeza, akanipa njia ya kufuatilia hadi mambo yakakaa sawa. Alikuwa kiongozi mwenye moyo wa kusaidia.”
Amesema vijana wa Iringa “wamepoteza mwamba,” mtu aliyekuwa akisimamia misingi ya utu, nidhamu na maadili.
Kwa ujumla, kauli za viongozi, wasanii, wafanyabiashara na wananchi zinaonyesha kuwa William Lukuvi alikuwa sio tu kiongozi wa serikali, bali pia mzazi wa jamii, mshauri wa vizazi, mtetezi wa wanyonge na mpenda maendeleo.
Urithi wake katika ardhi, miundombinu, elimu, siasa na ustawi wa jamii utaendelea kuwa rejea kwa vizazi vijavyo.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.