Na Beda Msimbe, TBN – Moscow
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University), huku akisema kuwa heshima hiyo ni ya Watanzania wote.
Shahada hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Oleg Yastrebov, katika hafla iliyofanyika chuoni hapo jijini Moscow, Urusi, tarehe 4 Juni, 2026.
Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika mageuzi ya sekta ya elimu, juhudi zake za kuimarisha diplomasia ya Tanzania, pamoja na mchango wake katika kukuza hadhi ya Tanzania kimataifa, hususan kupitia sekta ya utalii.
Akizungumza mara baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia alisema heshima hiyo si mafanikio yake binafsi, bali ni utambuzi wa juhudi, mshikamano na matarajio ya Watanzania wote katika kuijenga nchi yao.
Alisema shahada hiyo ni ishara ya kuthamini dhamira ya pamoja ya Watanzania katika kuleta maendeleo, ustawi wa binadamu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
“Nilipokea kwa furaha taarifa za kutunukiwa heshima hii, lakini mara moja nikatambua kuwa si yangu peke yangu. Ni heshima inayotambua dhamira yetu ya pamoja ya maendeleo, ushirikiano na ustawi wa binadamu,” alisema Dkt. Samia.
Hii ni shahada ya nane ya heshima kutunukiwa Rais Samia tangu aingie madarakani.
Aidha, Rais Samia alisema shahada hiyo ni ishara ya urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi na uthibitisho wa nafasi muhimu ya elimu katika kuunganisha mataifa.
Alisema heshima hiyo pia inaakisi uhusiano wa kudumu kati ya Tanzania na Urusi, nchi ambazo zimeendelea kushirikiana kwa miongo kadhaa katika sekta mbalimbali, hususan elimu.
Katika hotuba yake iliyosifiwa na Watanzania wanaoishi Urusi pamoja na viongozi wa vyuo vikuu nchini humo, Rais Samia alieleza kuwa kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa wakipata elimu nchini Urusi na kurejea nyumbani kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Alisema ushirikiano huo umeimarisha mahusiano ya watu wa mataifa hayo mawili na kuongeza urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Urusi.
“Mama amezungumza vizuri sana kuhusu Tanzania. Kupata mwaliko wa Rais Vladimir Putin kuja Urusi ni ishara kubwa ya kutambuliwa kwa Tanzania kimataifa. Hotuba yake imeonesha matumaini makubwa kwa taifa letu,” alisema Mwenyekiti wa Wanafunzi wa Tanzania nchini Urusi (TASCARU), Jeffrey Mashauri.
Naye Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Urusi, Pascal Gura, alisema Watanzania zaidi ya 300 wanaoishi nchini humo wamejivunia kupata nafasi ya kukutana na Rais Samia na kusikiliza maono yake kuhusu maendeleo ya Tanzania.
Katika hotuba yake, Rais Samia alieleza namna ambavyo Tanzania inaweza kufanikisha maendeleo makubwa zaidi kupitia mshikamano, ushirikiano na uwekezaji katika elimu.
Pia aliwakumbusha vijana umuhimu wa kujielimisha na kuzingatia falsafa ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyesisitiza kuwa maendeleo ya kweli lazima yaweke mwanadamu katikati ya kila jambo.
Aidha, aliwataka vijana kuitazama Tanzania kama taifa lenye fursa kubwa na kutumia taaluma zao kulijenga taifa kwa kuzingatia uzalendo, maadili na uwajibikaji.
Rais Samia alisema dokumentari iliyooneshwa kabla ya kutunukiwa shahada hiyo, iliyobeba mafanikio na maendeleo ya Tanzania, inaonesha dhamira ya kweli ya Watanzania katika kuijenga nchi yao.
Tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha RUDN miaka ya 1960, zaidi ya Watanzania 1,100 wamepata elimu katika taaluma mbalimbali kupitia chuo hicho. Idadi hiyo ni sehemu ya zaidi ya Watanzania 5,000 waliowahi kusoma nchini Urusi katika nyanja mbalimbali ikiwemo udaktari, uhandisi na sayansi.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alizungumzia makubaliano mbalimbali yaliyotiwa saini kati ya Tanzania na Urusi yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika elimu, utafiti na ufundishaji.

