Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya mazingira dunia Juni 5,2026 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imezindua bustani ya miti iliyopo eneo la Nkuhungu Swai Jijini Dodoma. 

Akizungumza baada ya uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Zuberi Homera Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Wizara ya Katiba na Sheria Nkasori Sarakikya, amesema utunzaji wa mazingira ni sehemu ya kulinda haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi katika mazingira salama na kupata chakula. 

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Pantience Ntwina ametoa wito kwa viongozi wa maeneo husika kuongeza ushirikiano katika jitihada za utunzaji wa mazingira na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Amesema baadhi ya maeneo yanayotekelezwa miradi ya upandaji miti yanakabiliwa na changamoto ya utupaji holela wa taka kutoka majumbani, hali inayochangia kuziba kwa mitaro na kuharibu mimea iliyopandwa katika maeneo hayo.

Naye Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi na uzalishajimali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba, amezitaka taasisi zinazojitolea kushiriki kampeni za upandaji miti kuacha tabia ya kupanda miti na kuitelekeza muda mfupi baadaye.

Mumba amesema licha ya taasisi zaidi ya 40 kujitokeza kushiriki kampeni za upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma, ni taasisi tatu pekee zilizofanikiwa kusimamia na kuitunza miti hiyo kikamilifu, zikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na STAMICO.

“Kampeni za upandaji miti zimekuwa zikifanyika mara nyingi lakini miti mingi imeshindwa kukua kutokana na kutelekezwa na taasisi zinazoanzisha kampeni hizo.Ni muhimu kila taasisi inayokuja kuomba eneo la kupanda miti iwe tayari kuitunza hadi itakapokuwa,” amesema Mumba.

Mpaka sasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika bustani hiyo imepanda takribani miti takribani 500.