Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akizungumza na wadau wa makaa ya mawe wakati wa kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, Machi 30, 2026.
Wadau wa makaa ya mawe wakimsikiliza Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akizungumza katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, Machi 30, 2026.
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa makaa ya mawe ni sekta muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, Katika kuimarisha uratibu na mshikamano wa sekta, Mhe. Mavunde amewahimiza wadau wa makaa ya mawe kuanzisha chama chao (association) kitakachowaunganisha ili kurahisisha shughuli zao na kushughulikia changamoto kwa pamoja kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza Machi 30, 2026 katika kikao na wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika jijini Dodoma, amesema kuwa mwaka 2024 sekta ya madini ilichangia asilimia 10.1 katika pato la taifa kabla ya kufikia malengo yaliyowekwa ya mwaka 2025, jambo linaloonesha kazi kubwa iliyofanyika. Aidha amebainisha kuwa biashara ya madini mwaka 2025 ilikua kwa asilimia 11.3 ambapo mchango mkubwa ulitokana na makaa ya mawe.
Pia amesema kuwa nchi imejaaliwa kuwa na rasilimali ya makaa ya mawe, hivyo kuna umuhimu wa kuangalia kwa jicho la kipekee mnyororo wa thamani ili kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha uchumi wa ndani. Ameongeza kuwa mahitaji ya ndani bado ni madogo kutokana na matumizi hafifu ya viwanda, huku zaidi ya asilimia 80 ya makaa ya mawe yanayozalishwa yakipelekwa nje ya nchi kuhudumia viwanda vya mataifa mengine.
Aidha amebainisha kuwa kuna ulazima wa kuweka mkakati wa kuhakikisha makaa ya mawe yanachangia katika maendeleo ya viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya madini mbalimbali.
Pia kwa Tume ya Madini kutokuwa na bei elekezi kwa Wafanyabiashara wa Makaa ya Mawe,
” kuanzia sasa hakutakuwa na bei elekezi itakayopangwa bila kuwashirikisha wadau”, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano na ushirikishwaji ili kupata uhalisia wa soko.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANCOAL Energies Ltd, Bw. Daniel Nikenze, amesema kuwa changamoto ipo katika namna ya uwasilishaji wa tozo ya royalty, ambapo TRA wanaihesabu kama pato la kampuni badala ya kodi inayokwenda serikalini.
Aidha amebainisha kuwa hali hiyo inaleta mkanganyiko katika mahesabu na kusababisha madai kwa migodi mingi.
Pia ameongeza kuwa kuna haja ya mamlaka husika kuoanisha mfumo huo ili kutambua royalty kama kodi halali, kwa kuwa mapato hayo tayari yanawasilishwa serikalini.
Kwa upande wake, Rahimi Rhanj amesema kuwa serikali inapaswa kuangalia mfumo tofauti wa uendeshaji wa sekta hiyo, akieleza kuwa baadhi ya nchi kama Australia na Afrika Kusini zinatumia mfumo wa mgawanyo unaoweza kuwa na manufaa zaidi. Aidha amebainisha kuwa soko la Uganda lina fursa kubwa ya ukuaji na linaweza kuongezeka maradufu, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya makaa ya mawe badala ya biomass katika viwanda.
Pia ameongeza kuwa kuwepo kwa mfumo mzuri wa tathmini ya royalty kutasaidia kukuza sekta ya makaa ya mawe na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

