
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki akizungumza katika Kongamano la Malkia wa Habari lililofanyika leo Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa Kongamano la Malkia wa Habari Penina Malundo akisoma taarifa ya kongamano hilo kwa mgeni rasmi Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki.

Mratibu wa Kongamano la Malkia wa Habari Penina Malundo (kushoto) akimkabidhi zawadi mgeni rasmi katika kongamano hilo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki.

Mharriri wa Habari Bakari Kimwanga akizungumza jambo katika Kongamano la Malkia wa Habari.

Mratibu wa Kongamano la Malkia wa Habari Penina Malundo (kushoto) akizungumza jambo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki.


Wanahabari Wanawake wakiwa katika mdahalo.

………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wanawake wanahabari nchini wametakiwa kujipanga ili kuendana na kasi ya mageuzi kidijitali katika kipindi ambacho sekta ya habari inapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia pamoia na kutumia fursa zilizopo kujijenga kitaaluma na kiuchumi.
Akizungumza katika Kongamano la Malkia wa Habari lililofanyika leo Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesisitiza umuhimu wa kongamano hilo kuwa chachu ya mabadiliko ya kweli, si tukio la kupita.
Mhe. Kairuki amesema kuwa ni umuhimu wa wanawake wanahabari kujenga uwezo katika maeneo mapya yanayochipua kwa kasi, ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, uchumi wa kidijitali na matumizi ya akili unde (AI), huku akieleza kuwa mustakabali wa uandishi wa habari unategemea uwezo wa kuendana na mabadiliko hayo.
Amebainisha kuwa ushindani katika sekta ya habari hauhitaji tena juhudi za mtu mmoja mmoja, bali unahitaji nguvu ya pamoja, ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuzalisha maudhui yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya kisasa.
Mhe. Kairuki amesisitiza kuwepo kwa mifumo ya kuwaendeleza wanahabari chipukizi, akieleza kuwa programu za usimamizi (mentorship) zinaweza kuwa daraja muhimu la kuhamisha ujuzi kutoka kwa wanahabari waliobobea kwenda kwa kizazi kipya.
“Ni muhimu kuimarisha ustawi wa taaluma, pia kuanzishwa kwa mifumo ya kifedha itakayowawezesha wanahabari kuwekeza katika miradi binafsi na kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoathiri kazi zao” amesema Mhe. Kairuki.
Kwa upande wake mratibu wa kongamano hilo, Penina Malundo amesema lengo la Kongamano hilo ni kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili waandishi wa habari wanawake, kushirikiana katika shughuli za kijamii na kusaidia kuinua sauti ya wanawake kupitia vyombo vya habari.
Katika Kongamano hilo waandishi wa habari wanawake walipata fursa ya kuchangia mada mbalimbali.
Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe, amehimiza wanahabari kujifunza mbinu za kukabiliana na taarifa hasi na kulinda taaluma yao katika mazingira ya kidijitali yanayobadilika kwa kasi.
Mhariri wa habari za siasa, Lilian Timbuka, amesisitiza umuhimu wa wanawake kujithamini na kuthubutu, hasa katika maeneo magumu kama uandishi wa uchunguzi, akibainisha kuwa uwezo wao haupaswi kutiliwa shaka.
Nae, mwandishi wa habari za biashara na takwimu, Aurea Simtowe, amesema kuwa mwelekeo wa sasa wa uandishi wa habari unahitaji uelewa mpana wa teknolojia, hususan AI, ili kurahisisha uchakataji wa taarifa na kuwafikia wasomaji kwa ufanisi zaidi.
Kwa ujumla, kongamano hilo limefungua ukurasa mpya unaoonesha kuwa uandishi wa habari hauko tena kwenye mfumo wa zamani, bali unahitaji ubunifu, ushirikiano na matumizi ya teknolojia ili wanawake wanahabari waweze kushindana na kufanikiwa katika zama hizi mpya.
