Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
SHIRIKA la Weka Mazingira Safi (WEMASA) limetoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wanawake ili kuwawezesha kuripoti kwa ufanisi zaidi masuala ya utunzaji wa mazingira na changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika jamii.
Mafunzo hayo yalitolewa kupitia warsha iliyofanyika leo March 11,2026 jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo wanahabari wanawake walipata fursa ya kujadili na kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mshauri mtaalamu wa masuala ya mazingira na mwakilishi wa taasisi ya Connect, Carlos Mdemu amesema wanahabari wana nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira na namna ya kukabiliana nazo.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa kila mtu huzalisha takribani kilo moja ya taka kwa siku, lakini sehemu kubwa ya taka hizo hazitupwi kwa njia sahihi jambo linalochangia kuenea kwa magonjwa pamoja na uharibifu wa mazingira.
Mdemu alieleza kuwa taka mbalimbali ikiwemo za kemikali na zile zinazooza sokoni zinahitaji kusimamiwa vizuri ili kuepusha madhara kwa binadamu na mazingira.
Ameongeza kuwa pamoja na changamoto zake, taka zinaweza pia kuwa fursa ya kiuchumi iwapo zitasimamiwa ipasavyo na kutumika kama malighafi katika shughuli za uzalishaji.
Ametolea mfano taka za plastiki ambazo hukusanywa na kuuzwa pamoja na taka za masokoni(taka zinazooza) zinazoweza kutumika kutengeneza mbolea au kufuga funza wanaotumika kama chakula cha kuku na samaki.
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, Jiji la Dar es Salaam huzalisha takribani tani 5,000 za taka kila siku huku sehemu kubwa ikitupwa au kushughulikiwa kwa njia zisizo rasmi, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto ya usimamizi wa taka.
Katika warsha hiyo, wadhamini mbalimbali akiwemo Taifa Gas na UTT AMIS walizungumza kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kulinda mazingira na afya za wananchi.
Meneja Uhusiano na Masoko wa Taifa Gas, Oscar Shelukindo amesema bado asilimia 9 hadi 10 tu ya Watanzania wanatumia nishati safi huku wengi wakiendelea kutumia kuni na mkaa.
Amesema changamoto kubwa ni gharama za awali za kununua mitungi pamoja na upatikanaji wa huduma hiyo katika baadhi ya maeneo, lakini kampuni hiyo imeanza hatua za kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi Mkoa wa Pwani ili kupunguza gharama.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi wa WEMASA, Ibrahim Haule alisema warsha hiyo imelenga kuwawezesha wanahabari wanawake kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira kwa kuelimisha jamii kupitia kazi zao za uandishi wa habari.




