Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sukari ya ABF ya Uingereza Bw. Paul Kenward, tarehe 11 Machi, 2026 Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sukari ya ABF ya Uingereza Bw. Paul Kenward, tarehe 11 Machi, 2026 Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
………….
Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amepokea salamu za António Guterres zilizowasilishwa kupitia Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Parfait Onanga‑Anyanga, katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari S. Machumu, Bw. Onanga-Anyanga yupo nchini kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.
Machumu amesema Mjumbe huyo maalum ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa unatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania baada ya matukio hayo, hususan uamuzi wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi pamoja na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa na kuendelea na mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa, sambamba na kuthamini mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.
Katika ziara yake nchini, Machumu amesema Bw. Onanga-Anyanga amekutana na viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama vya siasa.
Aidha, amekutana na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi pamoja na wadau wengine wa kisiasa na kijamii ili kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu matukio yaliyotokea na hatua zinazochukuliwa na Serikali.
“Bw. Onanga-Anyanga amesema mashauriano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kupata taswira halisi kuhusu uhalisia wa matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto zilizojitokeza,” amesema Machumu.
Kwa upande wake, Rais Samia ametuma salamu za shukrani kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutuma ujumbe maalum nchini Tanzania ili kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali.
Rais Samia amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki huku ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa.
Ameongeza kuwa Serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi mara baada ya kukamilika kwa kazi yake, akieleza kuwa mapendekezo hayo yatasaidia kuimarisha maridhiano ya kitaifa pamoja na mchakato wa marekebisho ya Katiba.
Pia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi nchini.
