Nchi za Afrika zimesisitizwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kukabiliana na changamoto za amani na usalama zinazolikabili bara hilo, zikiwemo ugaidi, itikadi kali na migogoro inayohatarisha utulivu na maendeleo.
Msisitizo huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Masuala ya Wamisri waishio Ughaibuni wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Dkt. Badr Abdelatty, Novemba 22, 2026, wakati wa Jukwaa la Sita la Aswan kuhusu Amani na Maendeleo Endelevu lililofanyika jijini Aswan, nchini Misri.
Katika jukwaa hilo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.), aliyeshiriki mijadala mbalimbali iliyohusu masuala ya amani na usalama, ikiwemo mjadala wa maendeleo na mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel.
Mjadala huo ulijikita katika umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiusalama, kubadilishana taarifa, kujenga uwezo wa taasisi za kikanda na kushughulikia sababu za msingi zinazochangia kuenea kwa ugaidi, zikiwemo umaskini na ukosefu wa ajira.
Aidha, kupitia Azimio la Aswan lililopitishwa Katika Mkutano huo, washiriki wameweka msisitizo katika kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za amani, usalama na maendeleo endelevu.
Jukwaa hilo limewakutanisha viongozi wa Afrika na washirika wa kimataifa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili bara hilo, huku likitoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.
Jukwaa la mwaka huu limefanyika Novemba 21 na 22, chini ya kaulimbiu isemayo “Redefining the Global Commons: Africa’s Agency in the Age of Disruption”, inayosisitiza nafasi ya Afrika katika kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kimataifa na kukabiliana na changamoto za dunia.

