Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema uwekezaji wa shilingi bilioni 434 katika ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, utakuwa suluhisho la changamoto ya kuchanganyika kwa shehena chafu na mizigo ya kawaida katika Bandari ya Mtwara, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora na thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi huo.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Jumapili, Novemba 22, 2026, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo, akieleza kuwa itakuwa mahususi kwa kuhudumia shehena chafu zikiwemo saruji, mbolea na makaa ya mawe, hivyo kuboresha ufanisi wa shughuli za upakuaji na upakiaji wa mizigo.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 na upana wa mita 40, huku akipongeza ubunifu wa Serikali wa kuanzisha tozo maalumu ya miundombinu (Infrastructure Fee), inayowezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya bandari na kurahisisha malipo kwa wakandarasi.

“Kwa mara ya kwanza unamuuliza mkandarasi, mkandarasi anasema sasa hivi ‘better’, hakuna shida. Tunaamini huko tutakokwenda mkandarasi atasema ‘best’ alafu atasema ‘excellent’. Kwa kweli suala la malipo halina shida,” amesema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa, “Value for money (thamani ya fedha) ndio kipaumbele chetu cha kwanza, halafu ubora wa kazi ni kipaumbele chetu cha pili kikubwa.”Alisema Mbarawa

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amesema uongozi wa mkoa na wilaya utaendelea kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo na kuomba mkandarasi kuwasilisha mpango kazi pamoja na ratiba ya utekelezaji ili kurahisisha ufuatiliaji. 

Ameeleza kuwa, kwa kuwa Serikali imeshatimiza wajibu wake wa kuhakikisha fedha zinapatikana, mkandarasi anapaswa kutimiza ahadi ya kufikia asilimia 85 ya ujenzi ifikapo Machi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Eric Madinda, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, amesema mradi umefikia asilimia 57 na unatarajiwa kufikia asilimia 85 ifikapo Machi, akibainisha kuwa bandari hiyo itaweza kuhudumia meli zenye uzito wa hadi tani 100,000 na kuhifadhi tani 205,000 za makaa ya mawe katika eneo la mita za mraba 52,000.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi na wabunge wa Mkoa wa Mtwara, Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini, Rashid Mohammed Mtima, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo akisema utafungua fursa za biashara, ajira na kukuza uchumi wa wananchi kupitia usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka Mchuchuma na bidhaa za saruji kutoka kiwanda cha Dangote, huku akieleza kuwa miundombinu wezeshi ikiwemo barabara na mikanda ya kusafirisha mizigo (conveyor belt) inafuatiliwa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Mradi huo unatarajia kukamilika Semptemba 2027.