Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha sekta ya uchunguzi wa kisayansi nchini baada ya kuiwezesha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kiasi cha shilingi bilioni 32.25 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kisasa ya maabara.
Mkemia Mkuu wa Serikali na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Fidelis Mafumiko, amesema hayo Machi 11,2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika miradi ya maendeleo pamoja na fursa kwa vijana kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema kuwa fedha hizo zimetumika kununua mitambo mikubwa ya kisasa 32 pamoja na vifaa vidogo vidogo 542 vitakavyosaidia kuongeza ufanisi katika huduma za uchunguzi wa kisayansi na kimaabara nchini.
Pia, Amebainisha kuwa uwekezaji huo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa mamlaka hiyo katika kuchunguza sampuli mbalimbali zenye changamoto na kutoa majibu ya uhakika kwa haraka zaidi, jambo litakaloongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari 2025 hadi Februari 2026, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanikiwa kufanya uchunguzi wa kisayansi kwa jumla ya sampuli 247,286 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Pia ameongeza kuwa uchunguzi huo umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya na hivyo kupunguza athari zake kwa vijana wa Kitanzania na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema kuwa utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha Januari 2025 hadi Februari 2026 umejikita katika maeneo makuu ikiwemo utoaji wa huduma za uchunguzi wa kimaabara, usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani, ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ofisi na maabara pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA.



