Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Angola Mheshimiwa João Lourenço pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika, tarehe 14 Februari, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

……….. 

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendeleza juhudi za kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kupitia mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa mataifa mbalimbali, kando ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari S. Machumu, mazungumzo hayo yamelenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji pamoja na kufungua fursa mpya za maendeleo kati ya Tanzania na mataifa husika.

Akinukuliwa katika taarifa hiyo, Bw. Machumu amesema kuwa tarehe 13 Februari 2026, Rais Dkt. Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Lourenço, ambapo viongozi hao walijadili kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, viwanda, nishati na miundombinu.

“Katika mazungumzo hayo, Rais Lourenço alikubali kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania na pia kuwa Mgeni Rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba mwaka 2026, hatua itakayochochea zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizi mbili,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa tarehe 14 Februari 2026, Rais Dkt. Samia alikutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali, ambapo walijadili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji pamoja na ushirikiano katika sekta za usafiri wa anga na usimamizi wa rasilimali za maji.

Kwa mujibu wa Bw. Machumu, viongozi hao pia walibadilishana uzoefu kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi zao, wakibainisha mikakati ya kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.

Halikadhalika, tarehe 15 Februari 2026, Rais Dkt. Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani, ambapo walijadili kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta za biashara, utalii, usafirishaji wa baharini na masuala ya usalama.

“Rais Assoumani alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa mchango wa Tanzania katika kuimarisha huduma za afya na usalama nchini Comoro, hususan kupitia huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wake,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imehitimisha kwa kueleza kuwa kupitia mazungumzo hayo, Tanzania inaendelea kujiimarisha katika jukwaa la Afrika na kimataifa kwa lengo la kukuza diplomasia ya kiuchumi na kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa.