Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akishiriki katika Mkutano wa Italia na Nchi za Afrika leo tarehe 13 Februari, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano huo uliwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika nyanja za kiuchumi, nishati na masuala ya kiusalama. 
…………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika wanaosimamia Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, Rais Samia alieleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta muhimu za uchumi zinazozalisha ajira ikiwemo kilimo, nishati, uvuvi, utalii na miundombinu, huku hali ya hewa isiyotabirika ikiendelea kudhoofisha mifumo ya maisha na uzalishaji barani Afrika.
Machumu alinukuu kauli ya Rais Samia akieleza mkakati wa Tanzania katika kukabiliana na changamoto hiyo, akisema unalenga kupanua upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuimarisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji katika vyanzo vya nishati jadidifu ikiwemo jua, upepo, jotoardhi na umeme wa maji endelevu pamoja na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, alisema Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni kipaumbele cha taifa kinacholingana na mwelekeo wa Afrika katika mageuzi ya sekta ya nishati, huku Tanzania ikiendelea kuchangia usalama wa nishati na mshikamano wa kiuchumi kupitia miundombinu ya pamoja ya kikanda.
Katika hatua nyingine, Machumu alimnukuu Rais Samia akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utabiri na usimamizi wa majanga kwa kushirikiana na taasisi za kikanda, akibainisha kuwa taarifa za hali ya hewa kwa wakati huokoa maisha na kupunguza gharama za kukabiliana na majanga, licha ya mifumo hiyo kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali.
Vilevile, alieleza kuwa Rais Samia alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa ahadi za kifedha za kimataifa kwa wakati na kwa ufanisi, akitaja taratibu ngumu, gharama kubwa za utekelezaji na utegemezi wa mikopo kuwa kikwazo kwa nchi zenye uwezo mdogo wa kifedha, hivyo kusisitiza umuhimu wa ruzuku na masharti nafuu ya fedha.
“Tanzania na nchi nyingi za Afrika zinahitaji ufadhili wa ruzuku na fedha za masharti nafuu ili kulinda mafanikio ya maendeleo huku zikikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alinukuliwa akisema.
Kadhalika, alisema Tanzania inaunga mkono Malengo ya Dunia ya Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi na inaendelea kushirikiana na ACMAD pamoja na taasisi nyingine za kikanda kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema.
Pia alimnukuu Rais Samia akiunga mkono juhudi za kuanzisha viwango vya pamoja vya Afrika katika masoko ya kaboni ili kuhakikisha biashara hiyo inaleta manufaa halisi kwa jamii na kulinda mazingira.
Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuongeza thamani ya rasilimali, madini ya kijani, utalii endelevu na miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya kujenga uchumi jumuishi unaozalisha ajira.
Kwa mujibu wa Machumu, Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi nyingine za Afrika katika maandalizi ya mikutano ijayo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha vipaumbele vya Bara vinapata msukumo wa kisera na kiutendaji.
Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika inayosimamia Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) ilianzishwa mwaka 2009 na Umoja wa Afrika kwa lengo la kuratibu msimamo wa pamoja wa Bara katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Tanzania ni miongoni mwa wanachama muhimu, ikiwa imewahi kuongoza Kamati ya Wataalamu na sasa ni mjumbe wa kudumu katika ngazi ya Wakuu wa Nchi.
