Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Februari 5, 2026
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Lailah Ngozi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni nguli na mbobezi wa siasa, kutokana na ujasiri na hekima yake ya kukiongoza chama kujisimamia chenyewe huku kikiendelea kusonga mbele kwa mafanikio.
Amesema Dkt. Samia ni mwanamke shupavu, mkomavu na mwenye dhamira safi ya kulitumikia Taifa, sifa zilizokiimarisha CCM na kuendelea kukifanya kuwa chama imara na chenye mwelekeo sahihi.
Akizungumza wilayani Rufiji mkoani Pwani katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM, Lailah Ngozi alisema chama hicho kipo katika mikono salama chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake Taifa.
Aidha, amewataka wanachama wa CCM kuendelea kulinda amani, kuimarisha mshikamano na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo, akisisitiza kuwa umoja na amani ya Watanzania ni nguzo kuu iliyoifanya CCM kuendelea kuongoza Taifa kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 49.
“Lindeni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo bila kuona aibu,” alisisitiza Ngozi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji, alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM katika sekta ya afya umeendelea kuimarika, huku Serikali ikiboresha miundombinu ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kuimarisha rasilimali watu kwa lengo la kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama za matibabu.
Katika kuhitimisha maadhimisho hayo ya miaka 49 ya CCM, viongozi wa Serikali na Chama, madiwani pamoja na wanachama wa CCM walifanya ziara ya kijamii katika Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Mji Rufiji, ambapo walitembelea na kuwafariji wagonjwa, hususan katika wodi ya wazazi, pamoja na kukabidhi zawadi kama ishara ya mshikamano na kujali ustawi wa jamii.





