10 January 2026
Kamati ya Uongozi ya Mkoa wa Mkoani wa Chama cha ACT Wazalendo imeendelea na ziara yake maalumu ya kuimarisha ujenzi wa Chama katika Jimbo la Chambani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha misingi ya Chama kuanzia ngazi za chini hadi juu.
Katika ziara hiyo, viongozi wa Mkoa walikutana na uongozi wa Jimbo pamoja na viongozi wa Matawi yote, ambapo walikumbushwa wajibu wao wa kuendeleza kwa kasi shughuli za ujenzi wa Chama, ikiwemo kuendesha vikao halali na vya mara kwa mara katika matawi na Jimbo, ili kuimarisha mshikamano, uwajibikaji na maamuzi ya pamoja.
Vilevile, ziara hiyo ililenga kutoa hamasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo, wakitambua nafasi yao muhimu katika mapambano ya kisiasa na mustakabali wa Zanzibar.
Viongozi walisisitiza kuwa nguvu ya Chama ipo kwa vijana wenye ari, ujasiri na maono ya mabadiliko ya kweli.
Aidha, wanachama walihimizwa kutokata tamaa wala kukata tamaa katika safari ya kudai haki, wakikumbushwa kuwa jitihada zao zinalenga kuipatia Zanzibar nusra ya kweli, yenye demokrasia, haki na maendeleo yanayomgusa mwananchi wa kawaida.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mwendelezo wa harakati za Chama cha ACT Wazalendo za kujijenga kwa misingi imara, kuimarisha uongozi wake na kujiandaa kikamilifu kwa mapambano ya kisiasa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.



