Na John Bukuku – Ikulu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemshukuru Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, kwa kutoa tuzo ya kutambua mchango wa Serikali ya Tanzania katika kukuza mpira wa miguu barani Afrika.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima ya wanamichezo wote waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, Januari 10, 2026, Rais Samia amesema jitihada, nidhamu na mshikamano uliooneshwa na wanamichezo hao ni alama ya uzalendo wa kweli na umeiwezesha Tanzania kupeperusha vyema bendera ya Taifa na kuandika historia mpya katika ulimwengu wa michezo.
Amesema kuwa Tanzania inapoelekea kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, jukumu lililopo mbele ya Taifa ni kubwa na linahitaji mshikamano wa kitaifa, maandalizi ya mapema pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa michezo.
Aidha, amebainisha kuwa ni wajibu wa Watanzania wote kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa heshima na manufaa ya Taifa, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji wazawa kwa kuwapa nafasi ya kucheza mechi nyingi za ndani ili kupata uzoefu, ushindani wa kutosha na maendeleo ya kitaaluma na kijamii.
Rais Samia amesema kuwa kuna umuhimu wa ushirikiano kati ya vilabu na wadau wa soka ili kuhakikisha ligi za ndani zinaendelea kuwa imara, shindani na kutoa fursa kwa wachezaji wazawa. Aidha, amesisitiza kuwa macho ya viongozi wa michezo yaelekezwe kwa vijana katika nyanja zote za michezo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa wito kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na TAMISEMI kuweka mikakati madhubuti ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo kuanzia ngazi za chini, ikiwemo mashuleni, mitaani na kupitia mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, amebainisha kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuwekeza katika michezo, hususan kupitia uanzishwaji wa vituo vya kukuza vipaji na akademia za michezo (Sports Academies), akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia uwekezaji huo kwa kutambua mchango wa michezo katika ajira, uzalendo na umoja wa kitaifa.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali inapanga kuanzisha na kuendeleza akademia za michezo pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya michezo nchini.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wanamichezo, kuwaunga mkono na kuwekeza katika maendeleo ya michezo ili kuongeza hamasa na kuendelea kuiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Rais Samia amezipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Taifa kwa usimamizi mzuri wa michezo nchini, na kusisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Habari ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Habari ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na vyama vya michezo.
Pia, amezipongeza wizara na taasisi zilizochangia mafanikio ya Tanzania katika sekta ya utalii, ikiwemo kutwaa tuzo mbalimbali za kimataifa, na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kubaki kitovu cha amani, michezo na utalii barani Afrika na duniani.




