……………..
NA JOHN BUKUKU, KAPRIPOINT MWANZA
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bwana Paul Kihongosi, amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka huu ni bora kuliko ilani yoyote iliyowahi kutolewa katika historia ya chama hicho, kwani imebeba matumaini makubwa ya Watanzania na kugusa kila kundi katika jamii.
Akizungumza katika kongamano lililozungumzia kampeni za Dkt. Samia Suluhu Hassan lililohusisha makundi mbalimbali ya kijamii na kufanyika Chuo cha Benki Kapripoint jijini Mwanza Katibu wa NEC Itikadi, Siasa na Mafunzo Chama Cha Mapinduzi amesema ilani hiyo imeandaliwa kwa umakini mkubwa kwa lengo la kuleta majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa makundi yote, wakiwemo vijana, wanawake, wazee, watoto, walezi, na watu wenye mahitaji maalum, huku ikiingia hadi ngazi ya familia.
“Ilani hii ni ajenda ya maendeleo na mapinduzi ya kiuchumi. Dkt. Samia anaijenga Tanzania mpya ambapo rasilimali zetu zinachakatwa kuanzia ngazi ya wilaya, na hatimaye kuleta manufaa kwa wananchi wote,” alisema Kihongosi.
Ameongeza kuwa, kupitia uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imeweka mkazo katika kuondoa kero ya maji, kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 8000 — mara mbili ya kiwango cha sasa — na kuboresha makazi ya wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya 60 za mikutano ya ana kwa ana kati ya Dkt. Samia na wananchi, Kihongosi alisema mikutano hiyo imekuwa jukwaa muhimu la mawasiliano yenye maelewano na imejenga matumaini mapya miongoni mwa Watanzania.
“Dkt. Samia amezunguka kila kona ya nchi hii yenye kilomita za mraba 947,743, akiwa na afya njema, nguvu na utayari wa kuendelea kulitumikia taifa,” alisema Kihongosi.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha kampeni, zaidi ya watu milioni 25.3 wamehudhuria mikutano ya moja kwa moja, huku milioni 57.1 wakifuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kwa ujumla, taarifa na matukio ya kampeni yamefikiwa mara 164.9 milioni kupitia redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii, simu na vifaa vya kidijitali katika maeneo mbalimbali kuanzia barabarani, nyumbani, hadi katika baa.
“Tumeshuhudia wananchi wakijitokeza kwa shauku kubwa kumsikiliza Dkt. Samia — hii ni ishara ya imani yao kwake, kutokana na utendaji wake thabiti katika kipindi cha miaka minne iliyopita,” alisisitiza Kihongosi.
Ameongeza kuwa Rais Samia amekuwa msikivu kwa wananchi, akiwapa nafasi ya kueleza changamoto zao, na hata kuunda timu maalum kupitia ofisi yake binafsi kwa ajili ya kushughulikia kero hizo.
Kihongosi aliwataka Watanzania wote kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu, akisema kitendo hicho kinadhihirisha uzalendo na uelewa wa haki zao za kikatiba.
“Ukipiga kura, unaonyesha kuwa wewe ni Mtanzania unayejua haki zako na unaijali nchi yako,” alisema Kihongosi.




