Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Kahe, Oktoba 11, 2025
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Enock Koola, amempongeza na kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa ahadi ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya urefu wa kilomita 31 kutoka Chekereni–Kahe hadi Mabogini.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kahe Magharibi, Mhe. Koola alisema ahadi hiyo ni ushahidi tosha wa dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwaletea maendeleo wananchi wa Vunjo na Tanzania kwa ujumla.
“Tunakushukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kutusikia na kutujali. Ahadi hii ya barabara ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Kahe, Chekereni na Mabogini. Tutakuhakikishia kura za kishindo Oktoba 29,” alisema Mhe. Koola huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Mhe. Koola aliahidi kutoa utumishi uliotukuka, wa uadilifu na uliosimikwa katika misingi ya maendeleo ya watu pindi atakapopewa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Vunjo. Alisisitiza kuwa barabara hiyo si tu itarahisisha usafiri na biashara, bali pia itachochea uchumi wa eneo hilo kwa kiwango kikubwa.
Katika mkutano huo, Mhe. Koola aliambatana na Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel, ambaye naye alitumia jukwaa hilo kupongeza jitihada za Rais Samia katika sekta mbalimbali, hususan afya, elimu na miundombinu.
Mhe. Mollel aliwahimiza wananchi wa Kahe Magharibi na Jimbo zima la Vunjo kuhakikisha wanamchagua Rais Samia kwa kishindo, sambamba na kuwachagua viongozi wa CCM, akiwemo Mhe. Enock Koola kwa ubunge, na Mhe. Abdul Msangi kwa udiwani wa Kata ya Kahe Magharibi.
“Tumeshuhudia mageuzi makubwa chini ya uongozi wa Rais Samia. Leo barabara za lami zinaingia hadi vijijini, vituo vya afya vina vifaa na dawa, na wanafunzi wanapata elimu bora. Haya yote yanahitaji kuendelezwa kupitia kura zenu,” alisisitiza Mhe. Mollel.
Mkutano huo ulimalizika kwa shangwe, nderemo na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi waliotoa ahadi ya kuwapa ushindi wa kishindo wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.