NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Mratibu wa Kampeni Kata ya Buhongwa, Rose Jacob Vicent, amesema kuwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamepokea kwa furaha kubwa ujio wa Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Uwanja wa Nyamagana kwa ajili ya kampeni za Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Ameyasema hayo Oktoba 7, 2025, katika muendelezo wa kampeni za chama hicho jijini Mwanza.
Amesema kuwa wananchi wa Mwanza wanafurahia kwa dhati kumpokea Mama Samia kutokana na mambo mengi aliyoyatekeleza katika Wilaya ya Nyamagana, na kwamba kampeni zinaendelea kwa kasi kupitia mfumo wa nyumba kwa nyumba, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29.
Aidha, Rose Jacob Vicent amebainisha kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi katika mapokezi hayo, wakionesha upendo na imani kubwa kwa Dkt. Samia, ambaye ameelezwa kuwa ni kiongozi mwanamke aliyethubutu na kuleta amani, utulivu na maendeleo nchini.
Amesema kuwa jambo kubwa alilolifanya Dkt. Samia katika Wilaya ya Nyamagana ni kuendeleza miradi iliyokuwa imeanzishwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ikiwemo ujenzi wa Stendi ya Buhongwa, Soko Kuu la Jiji la Mwanza, na madaraja mbalimbali yaliyokuwa katika hatua za mwisho.
Aidha, amebainisha kuwa miradi hiyo imekamilika kwa kiwango kikubwa na wananchi wameendelea kunufaika na maendeleo hayo.
Pia, amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia, wakiamini kuwa chini ya uongozi wake, miradi mingine mikubwa ya maendeleo itaendelea kukamilika kwa manufaa ya wananchi wa Nyamagana na Taifa kwa ujumla.