NA JOHN BUKUKU- KAZURAMIMBA- UVINZA
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwasaidia wanawake wajasiriamali wa Kazuramimba, wilayani Uvinza, hususan wale wanaofanya biashara kandokando ya barabara kuu ya Tabora–Kigoma, kwa kuwajengea maeneo bora na salama ya kufanyia biashara.
Dkt. Samia alisema leo Septemba 13, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Kazuramimba Uvinza mkoani Kigoma kuwa wanawake wauzaji wa mazao ndiyo uti wa mgongo wa familia na jamii, hivyo wanastahili mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao bila bughudha na bila kuhatarisha afya na usalama wao.
Amesema serikali yake itashirikiana na wabunge wa viti maalum kuhakikisha maeneo hayo yanajengwa kwa mpangilio mzuri.
Aidha, Dkt. Samia alibainisha kuwa serikali itaendelea kusaidia sekta ya kilimo na ufugaji kupitia ruzuku za mbolea, pembejeo na huduma za ugani, hatua itakayosaidia kuongeza tija na thamani ya mazao ya akina mama wa Uvinza.
“Nimeambiwa hapa Uvinza kina mama ni walimaji wakubwa wa maharage na wanachangia pakubwa kwenye uchumi wa kaya. Mbolea ya ruzuku, pembejeo na huduma za ugani zimewasaidia sana. Tutaendeleza ruzuku hizi kwa wakulima na pia wafugaji wa Uvinza ili kuongeza kipato na kuimarisha maisha ya familia zao,” alisema.
Ameongeza kuwa hatua hizi zitachochea maendeleo makubwa kwa wanawake na familia zao, na kuchangia kukuza uchumi wa wilaya kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia alitaja mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya CCM, yakiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya na zahanati, na ongezeko la upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 91. Pia ameahidi kujenga vituo vipya vya afya Kandaga, Kamera na Basanza pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto Businde na kituo cha afya Kazuramimba.
Kuhusu elimu, alisema serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 13 katika shule za msingi, bilioni 19 katika shule za sekondari na bilioni 2.8 katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), huku mpango wa elimu bila ada kuanzia chekechea hadi sekondari ukiendelea.
Aidha, alibainisha kuwa serikali imeunganisha kaya nyingi za Uvinza na umeme, kuanzisha viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao, sambamba na kusaidia wavuvi wadogo kupitia mikopo nafuu.
Dkt. Samia alimalizia kwa kusisitiza kuwa iwapo ataendelea kupewa ridhaa ya kuongoza nchi, serikali yake itaendeleza jitihada hizo na kuanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha Watanzania, hususan akinamama na familia zao, wananufaika na huduma za afya bila changamoto za kifedha.