Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele (kulia) akiwakabidhi seti moja ya fomu za uteuzi pamoja na nakala ya tamko la kuheshimu na kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Luhaga Mpina (54) na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais Fatma Alhabib Fereji (64) kupitia Chama cha ACT-Wazalendo leo, Septemba 13, 2025, katika Ofisi za INEC jijini Dar es Salaam.
Mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Luhaga Mpina (54) na Mgombea Makamu wa Rais Fatma Alhabib Fereji (64) kupitia Chama cha ACT-Wazalendo wakiwasili katika Ofisi za Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kurejesha fomu.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa kuwakabidhi seti moja ya fomu za uteuzi pamoja na nakala ya tamko la kuheshimu na kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Kwa wagombea wa Urais Chama Cha ACT – Wazalendo.
…….
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewateua Bw. Luhaga Mpina (54) kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Bi. Fatma Alhabib Fereji (64) kugombea nafasi ya Makamu wa Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Uteuzi huo umefanyika baada ya wagombea hao kutimiza masharti yaliyowekwa chini ya Ibara ya 39(1) na Ibara ya 47(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sambamba na Kifungu cha 34 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, kama ilivyofanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 1 ya mwaka 2024.
Akizungumza leo, Septemba 13, 2025, katika Ofisi za Tume huru ya Uchaguzi Jijini Dar es Salaam wakati wa kuwakabidhi seti moja ya fomu za uteuzi pamoja na nakala ya tamko la kuheshimu na kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele, ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni Ndogo ya 5 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, Tume imewateua rasmi Bw. Mpina na Bi. Fereji kama wagombea wa nafasi hizo kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mwambegele, amemuelekeza Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoa gari moja jipya aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya kampeni za mgombea urais, ili kuhakikisha usawa baina ya wagombea wote.
Hata hivyo, Chama cha ACT-Wazalendo hawakuwa tayari kutumia gari hilo, badala yake wameomba kuimarishiwa ulinzi katika kipindi chote cha kampeni.
