Mwamvua Mwinyi– Mkuranga
Julai 21,2025
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani, Muhidin Zakaria amekanusha vikali tuhuma za kusambaza kwa kura zilizopigwa kabla ya uchaguzi wa madiwani wa viti maalum uliofanyika Julai 20,2025 wilayani humo.
Zakaria alisema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba tayari mtu mmoja anayehusishwa na tuhuma hizo amekamatwa na kukabidhiwa kwa polisi kwa hatua zaidi.
“Hapa sina jina lake ila ameshafikishwa kwa vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi “
Alifafanua mtu huyo alikuwa miongoni mwa waliyeonyesha nia ya kugombea lakini jina lake halikuteuliwa kwenye orodha ya wagombea wa viti maalum vya udiwani.
Kwa mujibu wa Zakaria karatasi za kura alizokutwa nazo mtuhumiwa huyo ni tofauti kabisa na zile halali zilizotumika kwenye uchaguzi huo na kwamba lengo la tukio hilo lilikuwa labda kutaka kuchafua taswira ya chama.
“Ukiangalia ile karatasi ni feki iliyotengenezwa kwa lengo la analojua mwenyewe na ukiziangalia alizokuwa nazo na zilizotumika kupiga kura ni tofauti “anaongeza kusema Zakaria.
Taarifa hizo zilianza kusambaa baada ya video kuonekana kwenye mitandao ya kijamii ikionesha baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa wanachama wakilalamikia kile walichokiita usambazaji wa kura feki kabla ya muda wa uchaguzi.
Tukio hilo limeibua hali ya taharuki katika baadhi ya maeneo huku uongozi wa CCM ukisisitiza kuwa uchaguzi uliendelea kufanyika kwa amani na utulivu katika maeneo yote na kuwataka wanachama kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.