Hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya Sumbawanga Mh. Lilian Ndelwa wakati akiwaapisha Wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Rukwa na Katavi
Wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Rukwa na Katavi wakati wakila kiapo mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya Sumbawanga.
……………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:Wasimamizi wa uchaguzi kutoka ngazi ya mikoa na majimbo ya Rukwa na Katavi wameanza rasmi mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa RDC ulioko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuanzia leo Julai 21 hadi 23 ,2025.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na mjumbe wa tume huru ya taifa ya uchaguzi ambaye pia ni mgeni rasmi Magdalene Rwebangazira leo Julai 21, 2025.
Rwebangazira amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, uadilifu na uwazi ili kuwawezesha kuwajibika kwa weledi mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.
“Nawasisitiza kuepuka rushwa na malalamiko ya aina yoyote ambayo yako kinyume na maadili ya tume katika kipindi chote cha uchaguzi.” Amesema .
Aidha Rwebangazira amewasisitiza Wasimamizi hao kufanya kazi na vyama vyote vya siasa ambavyo vimepitishwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi bila upendeleo.
Wasimamizi hao pamoja na watendaji wote wanaohusika na uchaguzi wamekula kiapo cha kutunza siri na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Lilian Moses Ndelwa.
Mafunzo hayo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha demokrasia nchini kwa kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika kwa wote.
Kwa upande wake mmoja wa Wasimamizi wa uchaguzi kutoka katika Jimbo la Nsimbo mkoa wa Katavi Daniel Rafael amesema watayafanyia kazi yale yote waliyofundishwa na kufuata miongozo na taratibu za tume ya taifa ya uchaguzi.
“Nitahakikisha ninafanyia kazi maelekezo yote niliyopewa na kujiepusha na malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa zoezi la usimamizi wa uchaguzi na kusimamia Sheria za tume ya uchaguzi “.amesema Daniel.
