Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Benki ya NMB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuwa karibu na wananchi kwa kusogeza huduma zake moja kwa moja kwa wateja kupitia tawi maalum lililowekwa katika Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.
Akizungumza Juni 30, 2025, katika banda la benki hiyo, Mkuu wa Matawi na Mauzo wa NMB, Donatus Richard, alisema benki hiyo imejipanga kuwahudumia Watanzania wote – wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, vijana na wazazi – kwa kuwapatia huduma kamili za kifedha kama ilivyo katika matawi yao yote nchini.
“Hili si banda tu bali ni tawi kamili la benki. Wananchi wanaweza kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha, kupata mikopo, kujifunza namna ya kutumia huduma za kidijitali kama NMB Mkononi, na kupata elimu ya kifedha iliyo sahihi,” alisema Richard.
Amesema ushiriki wa NMB katika maonesho hayo ya 49 ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuhimiza ujumuishwaji wa kifedha, hasa kwa makundi yaliyo katika maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi na huduma za kifedha kama wakulima na wafanyabiashara wadogo.
“Tunatoa mikopo ya kilimo-biashara kwa njia ya kawaida na kidijitali, huduma za bima, na hata huduma za watoto – kuanzia akaunti za watoto wachanga hadi vijana wanaojifunza kuweka akiba,” aliongeza.
Richard amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza na kunufaika na huduma mbalimbali zilizoboreshwa, huku akisisitiza kuwa lengo kuu la NMB ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa kifedha.
Kwa kuendeleza huduma zake katika maonesho ya Sabasaba, NMB inadhihirisha kuwa benki hiyo ni mshirika imara wa maendeleo ya kiuchumi ya wananchi kwa vitendo – ikilenga si tu faida bali pia kuleta mabadiliko ya kweli kwa maisha ya Watanzania.