Timu ya Singida Black Stars imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba SC jioni ya leo Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.
Mabao yote ya Singida Black Stars yamefungwa na wachezaji kutoka Ghana, mshambuliaji Jonathan Sowah dakika ya 17 na kiungo Emmanuel Kwame Keyekeh mawili dakika ya 35 na 48, wakati bao pekee la Simba SC limefungwa na kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 49.
Bao la kwanza langoni alikuwa kipa Mguinea, Moussa ‘Pin Pin’ Camara, lakini akatoka nje dakika ya 25 baada ya kuumia kufuatia kugongana na Sowah – nafasi yake ikachukuliwa Ally Salim aliyeruhusu mabao mengine mawili ya Kayekeh.
Katika Fainali mwishoni mwa mwezi ujao – Singida Black Stars watakutana na Yanga SC ambayo katika Nusu Fainali iliitoa JKT Tanzania kwa kuichapa mabao 2-0 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.