Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleimani Jafo katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Watumiaji Duniani.
…………….
Dar es Salaam, Machi 21, 2025,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleimani Jafo, amezitaka taasisi zote za serikali zinazohusika na ulinzi wa mlaji kufanya kazi kwa pamoja kwa weledi ili kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa na mahitaji yao yanakidhiwa ipasavyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Watumiaji Duniani, Dkt. Jafo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mamlaka mbalimbali za udhibiti ili kuhakikisha bidhaa na huduma zinazopatikana zinakidhi viwango vya ubora na zinauzwa kwa bei nafuu.
Dkt. Jafo amezihimiza taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Vipimo (WMA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine muhimu kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha ulinzi wa walaji.
“Haki za watumiaji ni nguzo muhimu kwa ustawi wa uchumi wetu. Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa watumiaji wanalindwa dhidi ya unyonyaji, hasa katika mazingira ya mabadiliko ya soko la kimataifa,” alisema Dkt. Jafo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio, amesema kuwa FCC inaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda maslahi ya watumiaji na kuimarisha ushindani wa haki katika soko.
“Tunajivunia juhudi za kimataifa zinazolenga kulinda haki za walaji, na hapa Tanzania, tunahakikisha soko letu linakuwa la haki, uwazi na lenye ushindani wa kweli,” alisema Erio.
Aidha, alibainisha kuwa FCC imepata cheti cha Shirika la Uthibitisho la Kimataifa (ICO), hatua inayothibitisha jitihada za tume hiyo katika kupata utambuzi wa kimataifa na kujenga imani katika soko la Tanzania.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga, amepongeza FCC kwa juhudi zake katika kuimarisha ushindani mzuri kwenye sekta ya viwanda.
“Ni muhimu kwa viwanda vyetu kuendelea kuboresha bidhaa na huduma zao ili kukidhi matarajio ya watumiaji. Ushindani wa haki unaleta mazingira mazuri kwa biashara kukua huku tukihakikisha haki za watumiaji zinalindwa,” alisema Tenga.
Maadhimisho haya ya Siku ya Haki za Watumiaji Duniani yamekuwa jukwaa muhimu la kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika kulinda walaji na kutoa wito wa ushirikiano madhubuti kati ya serikali, wadau wa sekta binafsi na mashirika ya watumiaji ili kuimarisha mazingira ya soko la Tanzania.
Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani FCC Dkt. Aggrey Kalimwage Mlimuka
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio.