Kampuni ya MOIL imeonesha dhamira yake ya kuunga mkono mkakati wa Taifa wa nishati safi kwa vitendo, ikitazama fursa za kuwekeza katika uzalishaji wa Gesi Asilia iliyoshindikizwa (CNG) hapa nchini.
Akizungumza katika Kongamano na Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki (EAPCE’25), Mkurugenzi wa MOIL, Bw. Altaf Mansoor, aliishukuru Wizara ya Nishati kwa kuandaa jukwaa hilo muhimu, akisema limetoa fursa ya kujifunza na kujadili mustakabali wa sekta ya nishati.
“Kongamano hili limetupa mwanga kuhusu jinsi gani tunaweza kushiriki kikamilifu katika kusaidia juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali kwa ujumla katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na nishati mbadala kwa magari,” alisema Bw. Mansoor.
Aliongeza kuwa MOIL inatazama kwa makini uwezekano wa kuanza uzalishaji wa nishati hiyo hapa nchini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kulinda mazingira.
Kongamano la EAPCE’25 limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kwa siku tatu, wakijadili mbinu bora za uwekezaji katika nishati endelevu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.