Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aahidi suluhu ya changamoto za uvamizi na huduma za msingi
Dar es Salaam, Januari 17, 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, amefanya ziara katika kiwanda cha saruji Wazo Hill kilichopo Wilaya ya Kinondoni ili kushughulikia changamoto zinazolikumba kiwanda hicho. Ziara hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa uongozi wa kiwanda juu ya masuala ya uvamizi wa ardhi na changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu kama maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo, RC Chalamila alieleza kuwa changamoto ya uvamizi wa eneo la kiwanda imeathiri uzalishaji na mipango ya maendeleo ya kiwanda hicho, ambacho ni moja ya wawekezaji wakubwa mkoani Dar es Salaam. Aliongeza kuwa serikali ya mkoa imejipanga kuhakikisha kiwanda hicho kinaendelea kuchangia katika ajira na pato la taifa.
“Changamoto ya uvamizi wa ardhi ni lazima ishughulikiwe kwa haraka. Tumeagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuitisha mkutano wa pamoja kati ya wananchi wa eneo hili, uongozi wa kiwanda, pamoja na maafisa wa mkoa na wilaya ili kujadiliana na kufikia suluhu ya kudumu,” alisema RC Chalamila.
Kuhusu changamoto ya maji, Mheshimiwa Chalamila alimwagiza Mtendaji Mkuu wa DAWASA kufika kiwandani hapo mara moja kwa mazungumzo na menejimenti ya kiwanda ili kuhakikisha huduma za maji zinarudi katika hali ya kawaida.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Naibu Kamishna wa Ardhi Mkoa, wanasheria wa serikali, na Katibu Tawala wa Mkoa kuunda kamati ndogo itakayopitia nyaraka za kisheria na hukumu zilizotolewa kuhusu eneo hilo. Lengo la kamati hiyo ni kumpatia Mkuu wa Mkoa ushauri wa namna bora ya kushughulikia mgogoro huo kwa kuzingatia sheria na masilahi ya kiwanda.
Mheshimiwa Chalamila alisisitiza umuhimu wa kiwanda hicho, akibainisha kuwa ni moja ya waajiri wakubwa na chanzo muhimu cha mapato kwa taifa. “Ni jukumu letu kama serikali kuhakikisha wawekezaji kama hawa wanapata mazingira mazuri ya kufanikisha shughuli zao. Hili si tu kwa masilahi yao binafsi, bali kwa manufaa ya wananchi wote,” alihitimisha.
Ziara ya RC Chalamila imeonyesha dhamira ya dhati ya serikali ya mkoa kushughulikia changamoto zinazowakabili wawekezaji huku ikihakikisha wananchi wanashirikishwa katika maamuzi ya maendeleo.