Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Ubia wa Wadau wa Maji Kusini mwa Afrika (Global Water Partnership (Southern Africa & GWP Africa Coordination Unit), alishiriki Mkutano wa Bodi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo tarehe 13 Desemba, 2024, mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Miongoni mwa masuala mengine, mkutano huo wa mwisho wa mwaka ulijadili jinsi GWPSA inaweza kuongeza ufanisi na kupanua zaidi shughuli zake za kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu katika sekta ya maji kwa nchi nyingi zaidi barani Afrika.
Kama sehemu ya mikakati ya kufikia lengo hilo, GWPSA imepanga kushirikiana kwa karibu na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) pamoja na Serikali ya Afrika Kusini kuratibu maandalizi ya Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uwekezaji katika Sekta ya Maji (AIP), unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 nchini Afrika Kusini.
GWPSA inashirikiana na Umoja wa Afrika kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji Afrika, ambao unalenga kuongeza uwekezaji katika sekta ya maji barani kwa wastani wa Dola za Marekani bilioni 30 kila mwaka katika kipindi cha 2023 hadi 2030. Tanzania Bara na Zanzibar ni miongoni mwa wanufaika wa mpango huo.
Akiwa nchini Afrika Kusini, Rais Mstaafu alipata pia fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Pemmy Majodina, Waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira, kuhusu ushirikiano kati ya Serikali ya Afrika Kusini na GWPSA kuelekea maandalizi ya mkutano huo.