Na Prisca Libaga ,Arusha
WAJASILIAMALI Wadogo na wa Kati Afrika wamehimizwa kuwekeza Nchini Tanzania hususani sekta ya Utalii kwani ndio sekta yenye uhakika wa kipato.
Mbali ya kuwahimiza kuwekeza Nchini pia wajasiliamali hao wanawake na vijana wametakiwa kujisajili katika mfumo rasmi wa kifedha ili waweze kutambulika na serikali na benki ili waweze kukopesheka.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hanspaul,Sathir Singh Hanspaul katika Kongamano la tatu la Wajasiliamali Wanawake na Vijana Afrika lililoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali {NGO’S} la Accelerate Afrika Foundation na kuhudhuriwa wanawake na vijana 200 kutoka katika Nchi 20 Afrika lililofanyika Jijini Arusha.
Hanspaul alisema wakati umefika kwa Wajasiliamali wadogo na wa kati Wanawake na Vijana kufungua kampuni za kitalii ikiwa ni njia pekee ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliyefungua milango katika sekta hiyo kwa kuhimiza utalii kufuatia filamu yake ya The Royar Tour.
Alisema sekta ya Utalii kwa sasa ina fursa nyingi sana za kujiingizia kipato hivyo ni wakati wa wajasiliamali wadogo na wa kati kujikita katika sekta hiyo ni kuacha zana ya kutaka kuajiriliwa serikalini kwani serikali haiwezi kuajili wanawake na vijana wote katika nchi zao.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Hanspaul mbali ya kuhimiza hilo aliwataka Wajasilimali hao kuhakikisha wanasajiliwa katika mifumo rasmi ya kiserikali na kibenki ili waweze kutambulika na kukopeshwa na benki.
Alisema karne hii sio ya kufanya biashara kiholela ni lazima uwe katika mfumo rasmi wa kiserikali na uwe na nidhamu na matumizi ya fedha katika kibiashara na ukizingatia hayo hakika unaweza kufanikiwa katika maisha bila vikwazo.
Akifungua Kongamano hilo,Mratibu Mkuu wa NGO’S ya Accelerate Afrika Foundation, Pendo Lema alisema changamoto nyingi zinawakabili wajasiliamali wanawake na vijana katika kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kukosa mtaji wa biashara na wanafanya biashara bila kusajiliwa na taasisi za kiserikali hivyo kushindwa kutambulika serikalini na taasisi za kifedha.
Lema alisema kufuatia hali hiyo wameamua kuwakusanya wajasiliamali katika nchi hizo za Afrika ili kuwapa elimu ya umuhimu wa kujisajili serikalini na wakifanya hivyo ni rahisi kukopesheka katika taasisi za kifedha kwani hakuna mfanyabiashara aliyetoka kimaisha bila kukopa benki.
Naye Kyenekiki Kyando mwakili kutoka taasisi ya Bima ya Sanlam aliwahimiza wajasiliamali kuhakikisha wanakuwa na Bima katika Biashara zao kwani zinaweza kuwasaidia katika majanga mbalimbali ikiwemo Moto.