Mwakilishi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Msokolo Layya (katikati( akikabidhi msaada wa fimbo kwa mmoja wa watu wenye changamoto ya uoni katika hafla iliyofanyika Novemba 27, 2024 Zanzibar.
……………………………..
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
KAMPUNI ya Emirates Leisure Retail Zanzibar inayojishughulisha na utoaji wa huduma Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Zanzibar (AAKIA) imetoa msaada wa fimbo 50 kwa watu wenye changamoto ya uoni ili ziweze kuwasaidia.
Msokolo Layya ambaye ni mratibu wa tukio hilo la utoaji wa msaada huo akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kampuni hiyo Novemba 28, 2024 alisema tukio hilo sio la kwanza kwani wamekuwa wakishiriki katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika fukwe na huduma zingine za kijamii.
“Kampuni yetu imekuwa ikishiriki kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika uboreshaji wa mazingira pamoja na kuwasaidia watu wenye uhitaji na makundi maalumu,” alisema Layya.
Layya aliyataja makundi hayo kuwa ni ya vijana, walemavu na mahabusu.
Alisema kampuni hiyo ili wiwa kutoa msaada kwa kundi hilo lenye uhitaji kutokana na changamoto waliyo nayo hasa wanapokuwa kwenye shughuli zao za kila siku.
Layya alisema tukio hilo liliongozwa na Mkurugenzi anae shughulikia watu wenye ulemavu na kuwahusisha viongozi wa watu wenye chgangamoto ya uoni sanjari na wahisani ambao ni Kampuni ya Emirates wakiongozwa na Paul Attallah amoja na Ahmed Katrada kutoka Dubai.
Layya alitumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa Taasisi ya Al Ameen Foundation chini ya Mwenyekiti wake Ghalib Nassor Monero kwa ushirikiano na msaada mkubwa wa kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo kwa ajili ya watu wenye uhitaji maalumu.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu wasioona Zanzibar Fatma Djaa Chesa alisema msaada uliotolewa na kampuni hiyo ni mkubwa sana kwao na akaomba wasichoke kuwasaidia kutokana na uhitaji wao.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Ussy Khamis Debe aliwashukuru wadau wote waliotoa msaada huo.
“Msaada huu uliotolewa na Kampuni ya Emirates ni mkubwa mno nawaomba muendelee na moyo huo kwani na kuwashika mkono walengwa hao,” alisema Debe.
Viongozi mbalimbali wakibadilishana nawazo wakati wa hafla hiyo.
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi na kukabidhiwa msaada huo.