Aipongeza TARURA kwa mradi unaowawezesha wanawake na vijana
Dar es Salaam
Imeelezwa kwamba sekta ya kazi na usafirishaji ni baadhi ya sekta muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania.
Haya yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa hafla ya uzinduzi wa sehemu ya ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za vijijini kupitia vikundi vya kijamii- Community Based Routine Maintenance (CBRM) kupitia mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji wa Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) unatekelezwa na TARURA kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaama kwa ushirikiano wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Amesema kwamba ili kukuza maendeleo ya kiuchumi ya nchi inahitajika uwekezaji zaidi katika sekta hizo.
Aidha, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza sana katika miradi ya maendeleo hasa ile inayohusiana na miundombinu, hivyo kuwepo kwa barabara za vijijini na kufungua fursa za maendeleo vijijini ni jambo jema kwa wananchi.
“Katika utekelezaji wa mipango hii ya maendeleo ya miundombinu, ujumuishaji wa jamii katika ushiriki hususan wa vikundi vilivyo hatarini kupoteza matumaini ya kujikwamua kiuchumi imekuwa suala muhimu na miongoni mwa makundi ambayo yako katika hali ya hatari ni pamoja na wanawake,vijana na watu wenye ulemavu” Aliongeza.
Hata hivyo Mhe. Kikwete aliwapongeza TARURA kwa mradi huo unaowezesha wananchi wote haswa wanawake na vijana ambapo mradi huo utaacha urithi wa ufundi, uzoefu pamoja na kukuza ujuzi kwa kutengeneza wajuzi wenye fani mbalimbali.
“Niwapongeze TARURA na wadau wote kwa kuviwezesha vikundi hususan wanawake kwani mradi huu unaenda kuondoa mwanya wa jinsia baina yetu wanaume na wanawake vijijini” Alisisitiza
Naye, Mkurugenzi Mkazi wa ILO Ukanda wa Afrika Mashariki kwa Nchi za Tanzania, Burundi, Uganda, Rwanda na Kenya Bi. Caroline Mugalla amesema mradi huo unaenda kuwapatia nguvu makundi ya kijamii hususan wanawake na vijana.
Amesema ukiwashirikisha wenyeji wa eneo husika kwenye matengenezo ya barabara watawajibika kuweza kuhakikisha barabara zinatunzwa na kulindwa miongoni mwao kwenye jamii.
Wakati huohuo Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema mradi huo wa RISE ni mradi wa kipekee kwani unawahusisha wananchi wenyewe kuanzia kuchagua pamoja na utekelezaji wa mradi.
Amesema mradi huo unaenda kuwainua wananchi wa eneo husika kiuchumi kwani wanahusika moja kwa moja na hivyo kuwapatia fursa katika utekelezaji wa mradi huo.