Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea wataalamu wa hali ya hewa na uratibu wa maafa kutoka Uganda na Kenya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema dhidi ya majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.

Ziara hiyo iliyofanyika Juni 9, 2026 jijini Dodoma, imelenga kuwajengea uwezo wataalamu hao kwa kupata uzoefu kutoka Tanzania, ambayo ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika utekelezaji wa mifumo ya tahadhari za mapema barani Afrika.

Ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Agnes Kijazi, pamoja na Mtaalamu wa Tahadhari za Mapema kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), Dkt. Martin Brown Munene.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema mifumo ya tahadhari za mapema ina mchango mkubwa katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema matukio ya hali mbaya ya hewa yanaendelea kuongezeka kwa kasi pamoja na ukubwa wake, hali inayohitaji ushirikiano wa kikanda katika kuimarisha mifumo ya tahadhari na uratibu wa maafa.

“Mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda maisha na mali kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Kupitia ziara hii, wenzetu watajifunza namna bora ya kujenga, kutumia na kuratibu mifumo hiyo ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika ukanda wetu na Afrika kwa ujumla,” alisema Dkt. Chang’a.

Kwa upande wake, Dkt. Agnes Kijazi alipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na mifumo ya uratibu wa maafa.

Alisema Tanzania imeonyesha mfano mzuri wa ushirikiano na utekelezaji wa mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema, hatua inayosaidia kupunguza athari za majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Nawapongeza sana Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na uratibu wa maafa. Uzoefu huu utakuwa muhimu kwa nchi nyingine katika kuendeleza mifumo yao ya tahadhari za mapema,” alisema Dkt. Kijazi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kikanda za kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha jamii zinapata taarifa za mapema kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali mbaya ya hewa.