*NIRC Singida.
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kuboresha sekta ya kilimo nchini kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwani hatua zinazochukuliwa zitaboresha maisha ya Watanzania hasa wakulima.
Amesema Waziri wa. Kilimo Hussein Bashe anaitendea haki sekta ya kilimo na hakuna miujiza katika uchumi zaidi ya mapinduzi yanayofanywa sekta hiyo inayogusa watu wengi kupitia Umwagiliaji
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la mradi wa ujenzi skimu ya umwagiliaji Masimba kwa mkandarasi iliyopo kata ya Urughu wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza dira ya Rais kwa kuwahakikishia Watanzania kuwa na kilimo cha kisasa na kufanya mapinduzi ya kilimo kupitia sekta ya kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Magaharibi Mhe. Suleiman Mwenda amesema ni kilio cha muda mrefu kwa wakulima wa eneo hilo kuhitaji kuwa na kilimo cha umwagiliaji cha uhakika.
Amesema awali halmashauri ya wilaya ya Iramba Magharibi iliweka makadirio ya gharama za ukarabati wa bwawa la umwagiliaji katika skimu hiyo ambayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 2.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Miundombinu Mha. Raphael Laizer amesema mradi huo unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 10,496,185,520 ambapo utajumuisha ukarabati wa bwawa na sehemu ya utoro wa maji, Kuchimba mchanga na tope ndani ya bwawa ili kuongeza ujazo wa bwawa mita za ujazo 250,000, Ujenzi wa mfereji mkuu mita 200 kwa kiwango cha zege na Ujenzi wa mfereji wa upili mita 9,254 kwa kiwango cha zege.
Kukamilika ka ukarabati skimu ya umwagiliaji Masimba utanufaisha wakazi 24,000 wa Vijiji vitano ambavyo ni Masimba, Urughu, Mlandala, Mang’ole na Ujungu huku zao litakalolimwa ni mpunga pamoja na mbogamboga.