Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kigamboni Bw. Emmanuel Tarmo (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji ba Bodaboda Wilaya ya Kigamboni Bw. Patric Kayanda baada ya kuwajengea uwezo Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Kigamboni kuhusu kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya rushwa kwa jamii kuelekea katika uchaguzi Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, zoezi hilo limefanyika leo Novemba 22, 2024 katika Ofisi za TAKUKURU Kigamboni , Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kigamboni Bw. Emmanuel Tarmo akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Kigamboni
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kigamboni kwa kushirikiana na Maafisa Usafirishaji katika Wilaya hiyo wameanza kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya rushwa kwa kupandika mabango katika usafiri wa bajaji unaoeleza : Kuzuia rushwa ni jukumu langu na lako, tutimize uwajibu wetu “Tumia vyema fursa ya kuchagua au kuchaguliwa bila vitendo vya rushwa”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2024 Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kigamboni Bw. Emmanuel Tarmo, amesema kuwa maafisa wa usafirishaji wameamua kushirikiana na TAKUKURU kufikisha ujumbe wa mapambana dhidi ya rushwa kwa wananchi.
Bw. Tarmo amesema kuwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mtaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024 TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni wanajukumu kubwa la kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.
Amesema kuwa maafisa usafirishaji wamekuwa wakishirikiana na TAKUKURU kwa muda mrefu kama wadau muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kubeba ujumbe wa kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi.
“Maafisa Usafirishaji wamekuwa wazalendo kwa kujitolea kubeba ujumbe wa kuelimisha jamii kuzuia vitendo vya rushwa na wamekuwa wadau wetu muhimu sana” amesema Bw. Tarmo.
Bw. Tarmo amesema kuwa katika vyombo vya usafirishaji wanavyotumia wamebandika mabango yenye ujumbe unaoeleza : Kuzuia rushwa ni jukumu langu na lako, tutimize uwajibu wetu “Tumia vyema fursa ya kuchagua au kuchaguliwa bila vitendo vya rushwa”
Amesema kuwa ujumbe wa kuzuia rushwa katika uchaguzi unakwenda pamoja na ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unazungumzia haki ya kuchaguliwa na kuchagua pamoja na kushiriki zoezi la uchaguzi.
“Bajaji hizi zinapita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Kigamboni, hivyo wananchi wanasoma ujumbe wa kuzuia rushwa na kupata fursa uchagua viongozi katika uchaguzi bila kujihusisha na vitendo vya rushwa” amesema Tarmo.
Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji ba Bodaboda Wilaya ya Kigamboni Bw. Patric Kayanda, amempongeza Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni kwa kuwashirikisha katika zoezi la kutoa elimu kwa jamii ya kuzuia vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mtaa.
Amesema kuwa zoezi la kutoa elimu wamelipokea kwa mikono miwili na wanakwenda kulifanyia kazi kwa nguvu zote kwa kufata maelekezo ili kufikia malengo ya kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi.