Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dk Khalid Salum Mohamed akitoa hotuba ya makaribisho kwa Mgeni Rasmi katika hafla ya Uzinduzi wa Utiaji saini Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari iliofanyika Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akitoa hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa Utiaji saini Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari iliofanyika Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati akitoa hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa Utiaji saini Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari iliofanyika Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akitia saini hati ya Makubaliano katika hafla ya Uzinduzi wa Utiaji saini Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari iliofanyika Ikulu Zanziba. (PICHA NA YUSSUF SIMAI,MAELEZO ZANZIBAR,22/11/2024)
…….
Na Sabiha Khanis Maelezo 22.11.2024
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imejipanga kuboresha utoaji huduma za bandari ili kuongeza ufanisi kwa Taasisi zinazotoa huduma za bandari, Huduma za forodha na mamlaka za udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini.
Ameyasema hayo wakati wa utiaji saini na Uzinguzi wa Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari iliyofanyika Ikulu Zanzibar Mkoa wa Mjini Magharibi, amesema ili kuinua uchumi wa nchi ni vyema kuziboresha sekta muhumu ikiwemo Bandari.
Amesema Mpango huo una lengo la kuondosha urasimu kwa kupeana majukumu ya viashiria vilivyoandaliwa ndani ya mpango huo ili kuleta mageuzi ya kiutengaji katika utoaji huduma za Bandari.
Ameeleza kuwa mpango huo utarahisisha ushushaji wa makontena, kupunguza muda wa ukaaji wa meli ukutani, kusubiri ukuta pamoja na kupunguza muda wa utoaji wa mizigo bandarini na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za bandari ili kukuza uchumi wa nchi.
“Serikali imekusudia kuimarisha ukuaji wa huduma za bandari kwa kurahisisha upakiaji na ushushaji wa makontena katika bandari zote nchini” alifahamisha Dkt. Mwinyi.
Rais Mwinyi amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imedhamiria kuendesha huduma za bandari kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia kuwa bandari ndio mlango mkuu wa uchumi wa nchi katika kuingiza pato la Taifa.
Aidha Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa dhamira ya Serikali juu uandaaji wa Mpango wa Maboresho ya huduma za Bandari ni kuendelea kuifungua Zanzibar kiuchumi pamoja kupunguza gharama za kuagiza bidhaa nje ya nchi na kuongeza ufanisi kiutendaji.
Akielezea mikakati ya Serikali juu ya ukuzaji wa Uchumi Zanzibar unaendelea kwa kuwawekea wafanyabiashara mazingira bora kwa kuwajengea bandari jumuishi ya Mangapwani bandari ambayo itaweza kuhudumia meli kubwa za mizigo pamoja na meli za mafuta na gesi.
Aidha amewashukuru watendaji wa taasisi ya Tony Blair, Shirika la Bandari Zanzibar pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushrikiana na wadau wa bandari kuandaa mpango wa maboresho ya utoaji wa huduma za bandari ambao utaleta tija kwa taifa, pamoja na kuthamini juhudi zinazochukuliwa na washirika wa maendeleo, Taasisi Serikali na binafsi, wafanyabiashara kwa kuunga mkono mpango huo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Dkt. Mwinyi amewataka wadau wote wakiwemo Kampuni za uendeshaji wa bandari, Mamlaka za forodhaa, Mamlaka za Udhibiti wa Bidhaa zinazoingia Bandarini, Makampuni za utoaji wa Mizigo pamoja na Mamlaka zinazohusika na ulinzi na usalama Bandarini kuwa tayari kuutekeleza mpango huo kwa vitendo ili kuweza kufikia malengo.
Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed ameahidi kushirikiana kwa pamoja na wadau na taasisi zote zilizotia saini Mpango huo kuweka mfumo mmoja wa ufuatiliaji katika utekelezaji na kufanya tathmini ili kuongeza ufanisi na kuongeza tija nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis amesema mafanikio yamepatikana baada ya kuanza kwa maboresho ya sekta ya bandari kuingia mkataba na Kampuni ya Zanzibar Multiple ambayo yamepelekea kupunguza siku za kusubiri meli kutoka siku 40 hadi 20 na kufikia siku nane kwa mara ya kwanza kukua kiufanisi.
Amewataka wadau wa huduma za bandari kubadilika ili kwenda sambamba kiushindani na soko la bandari liliopo Duniani na kuleta ufanisi kiutendaji na kuongeza pato la Taifa.