Na WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Novemba 21, 2024 amekutana na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayewakilisha Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete aliyeambatana na Msimamizi wa Miradi ya Afya wa Benki ya Dunia Kanda Namba Moja ya Afrika Bw. Ernest Massiah kwa lengo la kujadiliana namna ya kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote.
Mkutano huo umefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Mhagama amesema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia umewezesha kupatikana maendeleo makubwa ya utekelezaji wa mpango ya uwekezaji wa afya ya mama na mtoto nchini (TMCHIP) ikiwemo kupunguza vifo pamoja na msaada wa kifedha na kiufundi unaotolewa na Benki ya Dunia.
Waziri Mhagama amesema ni muhimu kuanzisha mfuko wa wadau wa maendeleo (Multi-Donor Trust Fund) ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa endelevu na kuratibu misaada ya wafadhili katika kutekeleza ajenda za afya za muda mrefu kama Bima ya Afya kwa Wote, mpango jumuishi wa watumishi ngazi ya jamii (CHWs).
“Vilevile utaimarisha mifumo ya utayari wa kukabiliana na dharura, maafa, magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, tukikamilisha haya ushirikiano huu utakuwa mzuri zaidi kwakuwa hivi vyote ni vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ametoa shukrani kwa msaada wa Benki ya Dunia kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo amewahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano zaidi ili kutekeleza malengo ya Sekta ya Afya kwa manufaa ya watanzania wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayewakilisha Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete ameelezea furaha yake kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Dunia ambapo maendeleo makubwa yamepatikana kupitia mpango wa uwekezaji wa afya ya mama na mtoto (TMCHIP).
“Benki ya Dunia ina nia thabiti ya kuendelea kusaidia jitihada za Tanzania katika kuboresha sekta ya afya, Benki ya Dunia itafanya kila linalowezekana kuharakisha maandalizi ya mradi mpya wa dola za kimarekani Milioni 500 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI), mpango jumuishi wa watumishi wa afya ngazi ya jamii (CHWs) na kuimarisha mifumo ya utayari na kukabiliana na magonjwa ya dharura,” amesema Bw. Belete
Amesisitiza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuwa mshirika mkubwa na wa karibu kwa Tanzania katika kutekeleza ajenda za afya za kipaumbele pamoja na kuimarisha mifumo ya afya nchini ili kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa watanzania ikiwemo upatikanaji na uendeshaji wa mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.